Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Chabruma alainishwa mapemaaa

Ester Chabruma Pic Chabruma alainishwa mapemaaa

Sun, 10 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Kocha mkuu wa JKT Queens, Ester Chabruma amesema wachezaji waliokuwa kwenye majukumu ya timu ya taifa 'Twiga Stars' wamerejea kwenye mazoezi ya kujiandaa na Michezo ya Ligi Kuu ya Wanawake (WPL).

Takribani wachezaji 12 wa kikosi cha kwanza cha JKT walikuwa kwenye majukumu ya timu ya taifa iliyotolewa na Afrika Kusini kwa jumla ya mabao 4-0, ikipigwa nyumbani 3-0 kisha ugenini 1-0 kuwania kufuzu Mashindano ya Olimpiki.

Chabruma alisema idadi hiyo inajumuisha pia wale wa timu ya vijana chini ya miaka 20 waliokuwa wakishiriki mashindano ya ya All African Games yanayoendelea Accra, Ghana na kulikuwa na mapumziko mafupi kwa timu hiyo.

Aliongeza, Jumatatu iliyopita timu hiyo imeanza mazoezi kwa ajili ya mzunguko wa pili ambao utatoa hatma ya kutetea taji lao la ligi na hadi sasa katika michezo tisa iliyocheza ina pointi 19 ikiwa ni ya pili nyuma ya vinara Simba Queens yenye 25.

"Mzunguko wa kwanza umekuwa bora kwetu, tumeanza maandalizi kwa ajili ya kulinda tulichokuwa nacho na naamini mzunguko huu utakuwa bora pia kwetu," alisema kocha huyo.

Ni timu mbili pekee zinazoongoza kwa kufunga mabao mengi na kuruhusu mabao machache, ni Simba iliyofunga 33 na kuruhusu matano na JKT iliyofunga 31 na kuruhusu manne, zikifuatiwa na Yanga iliyofunga 16 na kuruhusu tisa, Ceasiaa Queens iliyofunga 11 na kuruhusu 11 na Fountain Gate Princess ikifunga 10 na kuruhusu 13 kwa timu hizo tano za juu kwenye msimamo wa ligi hiyo.

Chanzo: Mwanaspoti