Rais wa Shirikisho la Soka Ulaya (Uefa), Aleksander Ceferin amesema hatagombea kipindi kingine baada ya muda wake kumalizika mwaka 2027.
Kanuni mpya za Uefa ambazo zilipigiwa kura na kupitishwa jana mchana zinamruhusu Ceferin kugombea kipindi kingine ili kuliongoza shirikisho hilo ikiwa atataka kufanya hivyo.
Hii ina maana kuwa rais huyo ambaye alichukua nafasi ya Michel Platini ambaye alijiuzulu Mei 2016, angebaki madarakani hadi mwaka 2031, lakini amethibitisha kuwa hataki kugombea tena.
"Nilishaamua miezi sita iliyopita kuwa sitagombea tena, sababu ni moja tu, nafahamu baada ya kipindi kirefu taasisi yoyote ile inatakiwa kuwa na damu nyingine changa ili kuiendesha, lakini pia ni jambo gumu kwangu kuwa mbali na familia yangu kwa zaidi ya miaka saba," alisema Ceferin.
Hata hivyo, kanuni hiyo ya kuongeza kipindi kingine cha kugombea kwa rais aliyepo madarakani wa Uefa ilipingwa na FA ya England peke yake.