Kati ya makipa bora wazawa waliowahi kucheza Ligi Kuu Bara huwezi kuacha kulitaja jina la Hussein Shariff ‘Casillas.’
Enzi zake nyota huyo wa zamani wa Simba, Coastal Union, Kagera Sugar na Mtibwa Sugar alifananishwa na kipa wa zamani wa FC Porto, Real Madrid na Timu ya Taifa ya Hispania, Iker Casillas.
Casillas wa Bongo mwaka 2022 alikwenda kucheza soka la kulipwa Burundi katika timu ya Inter Star ya Ligi Kuu kwa mkataba wa mwaka mmoja.
Katika mahojiano na Mwanaspoti, kipa huyo anasema kwa sasa yupo nchini akitafuta timu ya kucheza baada ya mkataba wake kumalizika msimu huu.
“Nimecheza Burundi msimu mmoja nikaona nirudi kwanza nyumbani na kuna vitu nimejifunza kwenye ligi hiyo ikiwemo kupata marafiki wapya.
“Kila sehemu ina changamoto ili kukufanya uwe imara zaidi na naamini nilizopitia zinanifanya kujua kipi kizuri na kibaya,” alisema Casillas.
MALONE, MAXI WAMKOSHA
Casillas anasema wachezaji watatu waliosajiliwa Simba na Yanga ndio waliomkosha na anaamini wakiendelea na viwango hivyo watazisaidia sana timu hizo kimataifa.
Anamtaja beki wa kati wa Simba, Che Malone Fondoh, kiraka wa Yanga, Maxi Nzengeli na kiungo mshambuliaji Pacome Zouzoua kuwa ndio wachezaji wanaojua wamefuata nini Tanzania.
“Hawa wachezaji ni hatari mno na wanajitambua. Nimewaona kwenye baadhi ya mechi kikubwa waendelee kupambana,” aliongeza.
KWA MAKIPA
Kipa huyo anasema asilimia kubwa ya makipa nchini wanafanana aina ya udakaji na baadhi ya makosa wanayofanya, lakini mbali na kufanana kwao lakini wengi hawaaminiki kiasi cha kuwafanya hata wao wenyewe kutojiamini kama wanaweza.
“Makipa wengi wanaotoka nje ndio wanapewa kipaumbele sana. Hii inatokana na kutoamini vyetu na kuwafanya hata wao wenyewe kutojiamini. Naamini Tanzania kuna makipa wazuri, kikubwa tuwape nafasi na kuwasapoti,” alidai Casillas.
NGASA, KIPRE WALIMTESA
Wakati anacheza soka Tanzania, Casillas anasema kuna mastraika hasa wa timu kubwa ndio walikuwa wanamsumbua alipokuwa akikutana nao lakini kwa timu nyingine alikuwa hapati tabu.
Hapa anamtaja aliyekuwa mshambuliaji wa zamani wa Azam FC, Kipre Tchetche ambaye aliwahi kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2012/13 akiifungia mabao 17.
Wengine ni nyota wa zamani wa Yanga, Simba na Azam, Mrisho Ngassa na Saimon Msuva.
“Kuna washambuliaji nilikutana nao walijua kazi wanayo. Kwa hiyo wa timu kubwa ndio walikuwa wakinusumbua.”
YANGA, SIMBA CAF
Kipa huyo anazipa asilimia kubwa Simba na Yanga kutinga robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF) kutokana na ubora wa wachezaji. Anasema kutokana na ushiriki wa timu hizo mbili pamoja na ubora ziliouonyesha msimu huu utazifanya kupambana na kufikia malengo.
“Nafasi ya kwenda robo (fainali) zipo. Wana timu nzuri ni wao tu wafanye kazi kwa ufanisi na kwa utulivu wakijua malengo yao ni nini,” anasema.
MTIBWA HURUMA
Kwa kipa huyo anachokiona katika timu yake ya zamani ya Mtibwa Sugar kutofanya vizuri kwenye ligi ni kutokana na wachezaji kuchanganywa na matokeo mabaya waliyokutana nayo.
Anasema kwa sasa kinachotakiwa ni makocha kuwaweka sawa wachezaji kwa kuwa wana timu nzuri, lakini kukosa matokeo kunawagharimu.
“Timu ya vijana inafanya vizuri kuliko ile ya wakubwa. Nafikiri kuna shida kidogo ila naamini bado hawachelewa wajipange raundi ya pili watarudi kuinusuru timu,” alisema.
LIGI YA WANAWAKE
Casillas anasema Ligi Kuu ya Wanawake Bara kwa sasa inavutia na soka hilo ni bora kuliko la wanaume kutokana na jitihada za mabinti hao uwanjani.
“Kuna wachezaji wanacheza nje kama Clara Luvanga, Aisha Masaka, Opah Clement na wengine ambao hata ukiwaona wanavyopambana unaweza kusema sio Watanzania. Kwa hiyo tukiwapambania watafika mbali zaidi ya hapo.”
UBINGWA AZAM
Nyota huyo anasema hashangazwi na namna kikosi cha Azam FC kilivyo bora kwa sasa na ni timu inayoweza kufanya chochote.
Anasema kama Azam itaendeleza moto wake Ligi Kuu Bara hana hofu kwamba itachukua ubingwa msimu huu.
“Azam siku zote ni bora, ila kuna kipindi nilijiuliza kwa nini haifanyi vizuri? Wana wachezaji wazuri, uwekezaji bora na naona hata kocha wao ana misimamo. Wanapambana naona nafasi ya ubingwa iko kwao.”
MAJERAHA SIMBA
Mwaka 2015, Simba ilikuwa na makipa watatu Ivo Mapunda, Casillas na Manyika Peter Jr ambaye alipandishwa kutoka timu ya vijana. Ni kipindi ambacho Simba ilikuwa na wakati mgumu golini baada ya mastaa wawili kuumia kwa wakati mmoja.
Alianza Ivo kuvunjika kidole gumba na baadaye Casillas kuumia ugoko timu hiyo ilipoweka kambi Afrika Kusini ikijiandaa na dhidi ya Yanga.
Iliwalazimu mabosi wa Simba kumpeleka Ivo kambini huko wakati akiwa anaendelea na matibabu. Maneno mengi yaliibuka kwa wawili hao Ivo na Casillas, walikuwa hawaelewani baadaye kila mmoja aliamua kuondoka ndani ya timu hiyo.
“Nilibakiza mkataba wa mwaka mmoja Simba, sikuwa fiti, kwa hiyo nikawaomba viongozi wanitoe kwa mkopo Mtibwa ndipo nikaondoka, ushindani ulikuwa mkali kwani wote tulikuwa bora.
“Sikuwaza kuacha mpira, nilijua tatizo limekuja pia litapita kwa uwezo wa Mungu lakini kiukweli ilinifanya nianze upya na nilichanganyikiwa kiakili.
“Namheshimu sana kaka yangu Mapunda (Ivo), sijawahi kugombana naye lakini hata kwenye familia unakuta mtaelewana lakini kuna siku mtatofautiana, binadamu tuna mapungufu.”
UTANASHATI
“Mimi napenda kupendeza sana na hata vifaa vya michezo nanunua kwa gharama kubwa sana, mfano gloves za mkononi kuna muda nilinunua hadi Sh 300,000 kwa sababu naipenda kazi yangu kwa hiyo ili nifanye vizuri lazima nijiweke vizuri.
“Nanyoa kila baada ya wiki, kuna rafiki yangu anaitwa Dizo ndiye mara nyingi ananiambia niende kwake kunyoa,”
SOKA ANALIDAI
Casillas anasema “Bado natafuta kupitia mpira wa miguu kiufupi nalidai soka naamini kupitia hilo nitafanikisha mipango yangu mingi kwa kuwa tunatafuta,” anasema.
KIPINDI KIGUMU
“Baadhi ya wachezaji kutusingizia vitu kwa watu wengine ili tuonekane wabaya jambo ambalo lilikuwa linaniumiza sana wanasahau Mungu ndio anatoa rizki.