Jamie Carragher amesema Erling Haaland ni mchezaji wa fahari tu, huku akitaja mastaa watatu waliokuwa moto kwenye Ligi Kuu England kumzidi straika huyo wa Manchester City.
Haaland, 23, amekuwa kwenye wakati mgumu msimu huu kutokana na kushindwa kuonyesha makali kwenye mechi muhimu.
Licha ya kufunga mabao 30 katika michuano yote, straika huyo wa kimataifa wa Norway amekuwa hana muunganiko mzuri na wenzake uwanjani na matokeo yake anaiweka Man City kwenye mchuano mkali wa kuwania ubingwa wa Ligi Kuu England mbele ya Arsenal au Liverpool. Haaland ametoka kapa kwenye mechi zote dhidi ya mahasimu hao kwenye ubingwa.
Na alishindwa pia kuonyesha kiwango bora kwenye sare ya 3-3 dhidi ya Real Madrid kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Haaland kiwango chake kimeshuka, wakati msimu uliopita uliokuwa wa kwanza kwake England, alifunga mabao 52 na kuisaidia Man City kunyakua mataji matatu. Lakini, ukame wa mabao, umewaibua wakongwe wengi, akiwamo Carragher, aliyesema mchezaji huyo ni wa kifahari tu na si wa kumtegemea kwenye mechi muhimu.
Beki huyo wa zamani wa Liverpool alisema Haaland hatashinda Ballon d’Or kama hatabadilika staili yake ya uchezaji na kufanya mambo makubwa kwenye mechi kubwa, huku akisema mchezaji huyo hawafikii kabisa mastraika waliopata kuwa hatari kwenye Ligi Kuu England kama Thierry Henry, Luis Suarez na Harry Kane.