Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Cameroon tabu iko palepale

Cameroon National Team Cameroon tabu iko palepale

Thu, 25 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Si unaujua ule msemo wa utani kwamba ‘mtafika mbinguni mkiwa mmechoka sana’? Basi ndicho unachoweza kusema kuhusu Cameroon ambayo imeingia 16-Bora ikiwa imechoka sana baada ya kushinda 3-2 dhidi ya Gambia katika mechi ambayo mabao matatu yalifungwa ndani ya dakika tano za mwisho za mechi yao wa mwisho ya Kundi C la Afcon 2023.

Mabingwa hao mara tano wa Afrika, baada ya funga-nikufunge ya dakika za lalasalama, walipenya kwa kuwa na mabao mengi ya kufunga kwani walilingana kwa pointi na Guinea ambayo ilipigwa 2-0 na mabingwa watetezi Senegal.

Lakini habari mbaya ni kwamba licha ya kufuzu kwa taabu, bado shida iko palepale kwani kikosi hicho cha kocha Rigobert Song kitakabiliana na Nigeria katika mechi yao ijayo ya 16-Bora kwenye Uwanja wa Felix Houphouet Boigny Jumamosi (saa 5:00 usiku).

Ilikuwa mechi tamu na ya aina yake. Kipindi cha kwanza kiliisha bila bao kwa pande zote. Kipindi cha pili, Cameroon ilianza vyema ikapata bao la kuongoza katika dakika ya 56 kupitia kwa Karl Toko-Ekambi (ubao wa matokeo ukasomeka Gambia 0-1 Cameroon).

Gambia ikasawazisha kupitia kwa Ablie Jallow, (matokeo yakasomeka Gambia 1-1 Cameroon). Kisha katika dakika ya 85 Gambia wakaweka la pili kupitia kwa Ebrima Colley (matokeo yakasomeka Gambia 2-1 Cameroon).

Samuel Eto’o ambaye aliwaponda wachezaji wa diaspora wa Cameroon akisema hawachezi kizalendo ndio maana wako hatarini kuaga mapema Afcon, kamera zilimuonyesha akionekana kuchanganyikiwa jukwaani.

Lakini kumbe mechi ilikuwa haijaisha. Katika dakika ya 87, Cameroon wakasawazisha kupitia kwa beki wa Gambia, James Gomes ambaye alijiweka wakati akijaribu kuokoa na matokeo yakasomeka (2-2) na wakati ikidhaniwa mechi inaisha kwa sare, beki la Rennes ya Ufaransa, Christopher Wooh, liliruka hewani na kuweka ndonga mpira wa kona iliyochongwa na Georges-Kevin N’Koudou katika dakika ya 89 na kuandika bao la tatu na matokeo kusomeka (Gambia 2-3 Cameroon).

Ghafla, Cameroon walipata mshituko baada ya Gambia kupata kona katika dakika ya 93 na The Scorpions wakauweka mpira kambani, lakini ilipoangaliwa VAR ilibainika mfungaji alitumia mkono. Likakataliwa na Cameroon kupenya kwa taabu.

Guinea licha ya kufungwa 2-0 na Senegal, bado imesonga mbele kwa nafasi ya mshindi wa tatu aliyefanya vyema, ikiwa moja ya timu nne zilizopita kama ‘Best Loosers’.

ONANA AACHWA BENCHI Kulikuwa na dalili za kushangazwa na ‘underdogs’ Gambia ambayo imezidiwa na Cameroon kwa nafasi 80 za ubora wa viwango vya Fifa na ambayo ilifika robo fainali iliposhiriki Afcon kwa mara ya kwanza mwaka 2021.

Kocha mkuu wa Cameroon, Rigobert Song alimtema katika kikosi cha kwanza Andre Onana katika mabadiliko manne makubwa aliyoyafanya ya kikosi, huku langoni akimrejesha binamu wa kipa huyo wa Manchester United, Fabrice Ondoa.

Licha ya kuruhusu mabao mawili, kipa Ondoa alifanya kazi kubwa katika mechi hiyo iliyojaa ushindani ambayo mara mbili Cameroon waligongesha besela la Gambia. Ilikuwa mechi ya kukumbukwa!

Chanzo: www.tanzaniaweb.live