Kocha Mkuu wa CR Belouizdad, Marcos César Dias de Castro maarufu kama Marcos Paquetá (65) amesema kuwa katika mchezo wao wa kesho dhidi ya Yanga SC, atawakosa nyota wake watatu wa kikosi cha kwanza ambao hawatakuwa sehemu ya mchezo huo kutokana na sababu mbalimbali.
Bila kuwataja majina wachezaji hao wala nafasi wanazocheza, Mbrazil huyo amesema hayo wakati wa mkutano na wanahabari kuelekea mchezo huo wa makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika utakaopigwa kesho Jumamosi, Faebruari 24, 2024 katika Dimba la Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam kuanzia saa 1:00 jioni.
Aidha, Paquetá amesema anawaheshimu Yanga SC kwani wanayo timu nzuri na kocha mzuri hivyo kwenye mchezo wao wa kesho watacheza kwa tahadhari kubwa ili kufanikiwa malengo yao ya kufuzu kwenda robo fainali.
“Kesho nitawakosa wachezaji wangu watatu muhimu, lakini tunao mbadala wao ambao nao ni wachezaji wazuri tu. Kwa sababu nina ushindani mkubwa kwa wachezaji wangu kwenye kila nafasi, nina sub zenye uwezo wa juu kama wale ambao hawatacheza mchezo huo,”.