Kocha Mkuu wa CR Belouizdad, Marcos César Dias de Castro maarufu kama Marcos Paquetá (65) amesema kuwa anawaheshimu Yanga SC kwani wanayo timu nzuri na kocha mzuri hivyo kwenye mchezo wao wa kesho hawatajilipua badala yake watacheza kwa tahadhari kubwa.
Mbrazil huyo amesema hayo wakati wa mkutano na wanahabari kuelekea mchezo huo wa makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika utakaopigwa kesho Jumamosi, Faebruari 24, 2024 katika Dimba la Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam kuanzia saa 1:00 jioni.
"Yanga wana wachezaji wazuri na wana kocha mzuri ndiyo maana wamefanikiwa kufika hatua hii. Najua itakuwa ngumu kwetu kwa sababu ya hali ya hewa, tumetoka kwenye baridi, nyuzijoto 12°C mpaka 9°C, mvua zinanyesa sana.
"Unakuja hapa Tanzania unakuta unyevunyevu ni asilimia 70 mpaka 80, lazima ucheze kwa tahadhari sana, hatutacheza kwa kufunguka wala kushambulia lakini malengo yetu ni kufuzu kwenda robo fainali.
"Tunafahamu bado tuna nafasi kwenye mchezo mwingine wa mwisho, kila timu inatakiwa ijue hivyo kwamba bado ina nafasi kutokana na ugumu wa kundi letu, badala ya kujilipua kwenye mchezo wa kesho ni bora tukacheza kwa tahadhari kisha tutajua mchezo wa mwisho tunafanyaje," amesema Marcos Paquetá.