Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

CEO Mtibwa Sugar mguu nje, mguu ndani

CEO Mtibwar Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mtibwa Sugar, Swabri Aboubakar

Sun, 3 Dec 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Kichapo cha mabao 2-1 ilichopata Mtibwa Sugar kutoka kwa Tabora United umeufanya uongozi wa klabu hiyo ya Manungu wakianza kunyoosheana vidole huku wakimtaka Ofisa Mtendaji Mkuu, Swabri Aboubakar kujitathimini mwenyewe kabla ya kushukiwa kwa hali ilivyo klabuni hapo.

Taarifa za kuaminika kutoka ndani ya timu hiyo zililiambia Mwanaspoti, baada ya mchezo huo kuisha juzi usiku kilifanyika kikao cha kumtaka Swabri ajitathimini kabla ya hali haijakuwa mbaya zaidi ndani ya kikosi hicho kinachoburuza mkiani.

“Ni kweli ametakiwa kujiuzulu nafasi hiyo kwa sababu ameonekana amefeli hali inayoisababishia timu kufanya vibaya kwa msimu wa pili mfululizo, tunahitaji kujinasua kipindi hiki ingawa mwafaka juu yake haujafikiwa,” kilisema chanzo chetu.

Kwa upande wa Ofisa Habari wa Mtibwa, Thobias Kifaru alipotafutwa na Mwanaspoti kuzungumzia jambo hilo alisema ni wazi wao kama viongozi wanapitia kipindi kigumu cha matokeo mabaya hivyo ni wakati kwao wa kujifanyia tathimini wenyewe.

“Kwa bahati mbaya sikuwa na timu Tabora kwa sababu ninauguza mke wangu, suala la Swabri kutakiwa kujiuzulu kwa kweli hilo kwangu silifahamu, niwaombe mashabiki zetu tusinyoosheane vidole bali tuangalie jinsi ya kutoka tulipo,” alisema.

Hata hivyo, Mwanaspoti linatambua Swabri alitafutiwa mbadala wake ndani ya klabu hiyo ingawa alishindwa kupenya kutokana na kutoonekana mtu wa mpira huku viongozi wa wakitafuta mtaalamu zaidi atakayewatoa sehemu walipo na kuwapeleka juu. Katika michezo 11 iliyocheza Mtibwa imeshinda mmoja tu, sare miwili na kupoteza minane ikiendelea kusalia mkiani mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara na pointi tano huku ikiwa ndio timu pekee iliyoruhusu mabao mengi hadi sasa (23) na kufunga 11.

Chanzo: Mwanaspoti