Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

CECAFA U-18 Tanzania ilistahili kubeba ndoo

Tanzania CECAFA U18 CECAFA U-18 Tanzania ilistahili kubeba ndoo

Mon, 7 Aug 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Historia imeandikwa baada ya Timu ya Taifa ya Wanawake ya U-18 ya Tanzania kubeba ubingwa wa michuano ya nchi za Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) kwa kuifumua Uganda kwenye mchezo wa mwisho na kumaliza kileleni ikiwa na pointi 12.

Bao pekee lililofungwa dakika ya 41 na Winfrida Gerald, lililotosha kuipa heshima Tanzania Bara mbele ya Uganda ambayo ina rekodi ya kuzinyanyasa timu wenyeji kwenye michuano ya kimataifa ikiwamo ya soka la wanawake hadi la wanaume, lakini juzi kwenye Uwanja wa Azam Complex mambo yalienda tofauti.

Hii ni mara ya kwanza kwa michuano hiyo ianzishwe chini ya umri huo na wenyeji kufanya kweli kwa kubeba taji katika michuano iliyoshirikisha jumla ya nchi tano, zikiwamo Burundi, Ethiopia na Zanzibar.

Fainali hiyo ilibeba hisia kwa wapenda soka kwani timu zilishambuliana kwa wakati na kuonesha ugumu wa mechi hiyo, ndipo Winfrida akafanya kweli kufunga bao pekee la ushindi na kuifanya Tanzania Bara imalize na pointi 12 dhidi ya tisa za Uganda waliofukuzana nao tangu mwanzo.

Mshindi wa tatu ni Ethiopia ambayo ilimaliza mechi nne na kufanikiwa kukusanya point sita na mabao manane huku Burundi akipata ushindi wake wa kwanza kwenye mechi ya mwisho dhidi ya Zanzibar wa mabao 4-0.

Mwanaspoti linakuletea historia iliyoandikwa kwa mara ya Kwanza Tanzania Bara na matukio mbalimbali.

USHINDANI KWA WAGENI

Mbali na Tanzania Barakuweka rekodi ya aina yake lakini bado timu tano zilionesha ushindani wa hali ya juu.

Timu ya Uganda ilikuwa mfupa mgumu kwenye mashindano hayo kwani ilikuwa na mwendelezo wa kushinda mechi zake mfululizo na kuipa wasiwasi Bara kwa kuwa wote hawakupoteza na wala kuruhusu bao.

Kwenye michezo minne imeshinda mitatu dhidi ya Ethiopia bao 1-0, dhidi ya Zanzibar 3-0, dhidi ya Burundi 7-0 na mchezo wa mwisho kufungwa na Bara bao 1-0.

Ukitazama mechi zote utagundua ubora wa Uganda kila eneo hasa la kiungo kutengeneza nafasi na washambuliaji kuyageuza kuwa mabao.

Ethiopia ilifungwa michezo miwili na kupoteza bao 1-0 dhidi ya Uganda, na dhidi ya Bara mabao 2-0 lakini licha ya kufungwa michezo hiyo iliendelea kuonesha upinzani mkali kwa timu nyingine na mechi mbili za mwisho kushinda.

YABEBA TUZO TATU

Tuzo tano zilizotolewa na Cecafa kwenye mashindano haya Bara imebeba tatu ikiwemo kocha maalumu, kipa bora na mchezaji bora wa mashindano.

Kocha Bakari Shime amechukua tuzo ya kocha maalum kwa kuzisaidia timu za wanawake kufanya vizuri pamoja na kubeba kombe huku Husna Zuberi akichukua tuzo ya kipa bora kwa kulibakisha lango salama bila ya kuruhusu bao na mchezaji bora wa mashindano hayo ni Winifrida Gerald akibeba tuzo hiyo kwa kuipatia timu bao la ushindi pamoja na kuonesha uwezo mkubwa.

Burundi ilibeba tuzo ya timu yenye nidhamu kwani licha ya vipigo walivyopata haikuruhusu hasira wala fujo kuanzia kwa wachezaji wake, kocha na benchi la ufundi.

Huku Emush Daniel wa Ethiopia akiibuka na tuzo ya ufungaji bora akitupia mabao matano kwenye mechi mbili ‘hat trick’ moja na mabao mawili.

MABAO 14

Kama kuna raundi iliyoshuhudiwa mabao mengi zaidi ni ile ya tatu ambayo kwenye mechi mbili iliruhusu mabao 14.

Mechi ya kwanza saa 9 alasiri kati ya Ethiopia ambayo ilishinda mabao 6-1 huku baadaye saa 12 kamili jioni Uganda ikimtandika Burundi mabao 7-0.

Tangu michezo ya kwanza hii inakuwa raundi ya kwanza kushuhudia mabao mengi zaidi kwani mabao mengi yaliishia matatu kwenye michezo mingine.

HAT-TRICK MOJA

Hat trick ya Emush Daniel wa Ethiopia dhidi ya Zanzibar inaweka rekodi ya aina kwani kwenye mechi zote nne ndio pekee iliyofungwa.

Mchezaji huyo pia licha ya kufunga hat trick kwenye mchezo timu yake iliondoka na ushindi wa mabao 6-1 dhidi ya Zanzibar lakini amebeba tuzo ya mfungaji bora akiwaacha nyuma akina Aisha Juma wa Bara aliyekuwa na mabao matatu, Mahelet Bekele wa Ethiopia, Winifrida Gerald wa Bara, Phionah Nabulime na Kamiyati Naigaga wa Uganda wote wakifunga mabao mawili.

ZANZIBAR INA KITU

Mbali na Zanzibar kuruhusu mabao 14 kwenye mechi nne na kufunga bao moja pekee lakini bado timu hiyo ina kitu na ikiendeleza ilipoishia itasogea kwa namna moja ama nyingine.

Kwenye mechi hizo nne Zanzibar imefunga bao moja pekee lililofungwa na Hawa Juma kwa mkwaju wa penalti dakika ya 22 mchezo dhidi ya Ethiopia iliopoteza 6-1.

Zanzibar haina uzoefu na mashindano hayo lakini bado kuna baadhi ya mechi ilipambana na kuwashangaza watu.

Pengine kuanzishwa kwa Ligi ya Wanawake Zanzibar kutaisaidia angalau timu kupata uzoefu na mashindano mbalimbali.

Kocha wa kikosi hicho, Abdulmutik Haji anasema mbali na kuruhusu mabao hayo lakini timu yake inazidi kuimarika siku hadi siku.

Kocha huyo anasema hapo awali Zanzibar ilikuwa inafungwa mabao 14 katika mechi moja, hivyo mabao hayo katika mechi nne ni hatua nzuri kwao kwakuwa hawana ligi wala mashindano mengine.

“Sisi tunashukuru kwa kumaliza mashindano haya salama na kama kocha na wachezaji wangu tumejifunza kitu na Mwenyezi Mungu akijaalia mashindano mengine tutafanya vizuri na hii ni hatua nzuri kwetu kufungwa mabao haya,” alisema Haji

MSIKIE KARIA

Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia anasema ushindi wa Tanzania Bara unaipa taswira ya kuwa soka la wanawake nchini linakuwa lakini wao kama viongozi watahakikisha na Zanzibar nayo inasogea kidogo.

Karia anasema Bara imeanza kupata uzoefu, hivyo kilichobaki ni kuisukuma pia Zanzibar nayo ifikie malengo.

“Huu ni mwanzo mzuri kwa Bara na niwapongeze wachezaji na kocha kuhakikisha wanapata matokeo mazuri lakini kipekee mashabiki waliojaa uwanjani ambao wamepambana na kuwapa hamasa wachezaji wetu ila bado kidogo kwa wenzetu Zanzibar hawapo vizuri tunaenda kupambana nalo,” alisema Karia

SKUDU KAMA WOTE

Mbali na kupata kushuhudia mbungi likipigwa na wadada wa nchi tano lakini tumeshuhudia pia utaalamu na ufundi wao wa kucheza muziki na kuongeza idadi ya akina Skudu.

Mchezaji na winga mpya wa Yanga, Mahlatse Makudubela ‘Skudu’ wakati anatambulishwa na klabu hiyo ujio wake ulikuwa wa tofauti kwa kusindikizwa na muziki wa Amapiano.

Huku kwa wanawake Timu ya Taifa ya Ethiopia nao tumewashuhudia akina Skudu kibao ambao mbali na kucheza mpira wana utaalamu wa kucheza muziki na kuwapa burudani mashabiki.

MASHABIKI

Kwasasa soka la wanawake linazidi kukua nchini na hilo linadhihirika kupitia kwa mashabiki.

Mechi ya fainali imekuwa na mvuto na moja ya kitu kilichochagiza Tanzania Bara kupata ushindi huo ni kutokana na uwepo wa mashabiki.

Uwanjani kulikuwa na nyomi la mashabiki wa Tanzania ambao hawakuchoka kushangilia timu yao mpaka pale kipyenga cha mwamuzi kilipopulizwa kuhitimisha mechi hiyo.

Chanzo: Mwanaspoti