Klabu ya Raja Casablanca ya nchini Morocco imeiahushia kipigo tena Klabu ya Simba baada ya kuitungua mabao 3-1 katika Dimba la Mohammed wa V katika mechi ya Kundi C ya Kombe la Mabingwa Afrika.
Katika mchezo huo wa kukamilisha hatua ya makundi uliopigwa saa 4:00 usiku kwa saa za Morocco, sawa na saa 7:00 kwa saa za Tanzania, Raja ndio walikuwa wa kwanza kupata bao dakika ya 44 kupitia kwa Hamza Khabba kabla ya Jean Baleke kuisawadhishia Simba dakika ya 48, kipindi cha pili.
Raja walicharuka na kuongeza mashambulizi ambayo yaliwasaidia kupata bao dakika 70 kwa mkwaju wa penati kupitia kwa Hamza Khabba baada ya beki wa Simba Joash Onyango kufanya madhambi ndani ya eneo la hatari.
Dakika ya 89, Raja walipata bao jingine la tatu kupitia kwa Mohammed Boulascout na kufunga ukurasa wa mabao ambapo bao 3 hizo zimetosha kupeleka kilio Msimbazi.
Kwa matokeo hayo Raja imehitimisha hatua ya makundi bila kupoteza mchezo ushindi ×5 sare ×1 huku Simba SC ikipoteza mechi zote mbili dhidi ya Raja kwenye Kundi C licha ya timu zote mbili kufuzu kwenda hatua ya robo fainali.
FT: Raja Casablanca 3-1 Simba SC
⚽️ Hamza Khabba 44' 70'P
⚽️ Jean Beleke 48'
⚽️ Mohammed Boulascout 89'
Beki wa Simba, Joash Onyango amesababisha penati 3 mpaka sasa kwenye mashindano hayo katika maeneo ya kulia, kushoto na katikati. Penati moja kwenye mecchi dhidi ya Horoya na mechi zote mbili dhidi ya Raja (Dar es Salaam na Morocco).
MSIMAMO KUNDI C
1. Raja CA — 16
2. Simba SC — 9
3. Horoya AC — 7
4. Vipers SC — 2
Droo ya Hatua ya Robo Fainali inatarajiwa kupangwa Aprili 5, 2023 ambapo mechi zitachezwa Aprili 21 na 22 kisha marudio Aprili 28 na 29, 2023.