Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) iliyoketi juzi huko Rabat, Morocco imeamua kufuta hatua ya mwisho ya mchujo ya mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika, uamuzi ambao unaoweza kuwa wa asali au shubiri kwa klabu tofauti kutoka nchi wanachama wake.
Mbali na kufuta hatua hiyo, CAF imeamua pia hakutokuwa na fursa kwa timu zinazotolewa katika raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika ya kuingia katika Kombe la Shirikisho Afrika kama ilivyokuwa awali.
Ni uamuzi ambao hapana shaka utapokelewa kwa mikono miwili na bashasha kubwa na timu ambazo zitawakilisha nchi zao katika Kombe la Shirikisho Afrika ambazo kwa sasa zitalazimika kucheza raundi mbili tu ili ziweze kutinga hatua ya makundi tofauti na hapo mwanzo ambapo zilicheza raundi tatu za awali.
Lakini pia furaha nyingine ya timu hizo ni kupunguza mzigo wa ushindani ambao zimekuwa zikiupata kutoka katika timu zinazotolewa katika Ligi ya Mabingwa Afrika na kuangukia katika mashindano hayo.
Wakatihali ikiwa hivyo kwa timu za Kombe la Shirikisho, uamuzi huo hapana shaka ni mchungu kwa zile ambazo zitashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika kwani sasa hazitokuwa tena na nafasi ya kujitetea iwapo zitashindwa kufanya vizuri kwenye raundi ya kwanza ya mashindano hayo ambapo sasa zitajikuta zikiaga rasmi mashindano ya klabu Afrika.
Taarifa iliyotolewa na CAF juzi haikueleza sababu zilizopelekea kuchukuliwa kwa uamuzi huo ingawa imesisitiza kuwa utaanza kufanya kazi katika msimu ujao wa 2023/2024.
"Kamati ya utendaji pia imethibitisha kufutwa kwa hatua ya pili ya ziada ya awali ya Kombe la Shirikisho Afrika. Hii inamaanisha timu 16 zitazoshinda hatua ya pili ya awali zitafuzu kuingia hatua ya makundi katika Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2023/2024.
Kanuni ya uwepo wa raundi hiyo ya mwisho ya mchujo, imedumu kwa miaka 19 ambapo imedunmu tangu mashindano hayo yalipoanza kuchezwa rasmi mwaka 2004 baada ya kuunganishwa kwa Kombe la Washindi Afri pamoja na Kombe la CAF ambapo timu kadhaa zilizowahi kutolewa katika Ligi ya Mabingwa Afrika zimewahi kuyatumia vyema kwa kutwaa ubingwa ama kufika hatua ya fainali.
Tangu 2004 hadi sasa, timu sita zimechukua ubingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika kwa nyakati tofauti baada ya kutolewa katika Ligi ya Mabingwa Afrika ambazo ni Hearts of Oak ya Ghana, FAR Rabat(Morocco0, Etoile du Sahel (Tunisia), Al Ahly (Misri), TP Mazembe (DR Congo) na Raja Casablanca (Morocco).
Zilizowahi kufika fainali ni timu 10 ambazo ni TP Mazembe na AS Vita (DR Congo), Etoile du Sahel na Club Africain (Tunisia), MO Bejaia (Algeria), Djoliba (Mali), Sewe Sports (Ivory Coast), Dolphins (Nigeria), FFAR Rabat (Morocco) na Yanga ya Tanzania.
Mchezaji wa zamani wa Yanga,Edinily Lunyamila, alisema kuwepo kwa sheria hii mpya kwake anaona ni sawa kwami kutawafanya wachezaji na vilabu kwa ujumla kujua ni nini wanatakiwa kufanya na kwa wakati gani.
"Hii ni kanuni inayojenga ukizingatia inakwenda kuimarisha wachezaji wetu namna ya kutumia nafasi vizuri kwani watakuwa makini kuilinda fursa waliyomayo ili wasikubali kushindwa," alisema Winga huyo wa zamani.
Mshambuliaji wa zamani aliyewahi kuichezea Simba na Yanga Zamoyo Mogela alisema kwa upande wake hii sheria inakwenda kukuza soka la Tanzani kwani hakuna nafasi mbili tena bali moja tu na hawataitumia vibaya.
"Soka linakwenda kiushindani na sheria zinabadilika wachezaji wakaze buti ili wapate matokeo mazuri kwenye mashindano makubwa kama haya, kupitia mabadiliko haya mkazo utaongezeka na uwezo utaonekana," alisema Mogela.