Kiungo nyota wa Simba, Rally Bwalya ameliambia Mwanaspoti kwamba baada ya kuondoka kwa Luis Miquissone na Clatous Chama amepewa majukumu makubwa katika kikosi haswa timu hiyo inapokuwa inafanya mashambulizi.
Anasema hicho ndicho kinachomfanya aonekane kung’ara zaidi kwenye michezo ya siku za hivi karibuni. Anasema benchi la ufundi limempatia maagizo ya kiufundi kuwa mchezaji ambaye muda mwingi anahusika na mpira pindi Simba inaposhambulia kama si kupiga pasi ya mwisho basi kufunga.
“Ndio maana mpaka sasa nimefunga mabao mawili katika mechi mbili za kimashindano lakini nimehusika katika mabao mengine tuliyofunga katika Ligi Kuu Bara na mshindano ya kimataifa,” amesema Bwalya aliyefunga bao katika mechi ya Jwaneng Galaxy na Polisi Tanzania ambalo lilikuwa la ushindi.
Bwalya ambaye ni Mzambia, hakuishia hapo amesema malengo yake makubwa msimu huu ni kuhakikisha timu inafanya vizuri na katika kukamilisha hilo maana yake anatakiwa kutimiza yale majukumu aliyopangiwa.
Anasema atahakikisha anapata nafasi ya kucheza katika kila mechi na atakuwa anahusika katika mabao ikiwezekana kupiga pasi za mwisho kwa wachezaji wengine au kufunga zaidi ya sasa na akawataka mashabiki wa Simba kuwa na imani na timu yao badala ya kuwakatisha tamaa.
“Unajua kuziba mapengo ya Chama na Luis kwa haraka si kitu rahisi, lakini kutokana na usajili uliofanyika nina imani kuna makubwa yanakuja,” amesema Bwalya ambaye awali alikaribia kutua Yanga.