Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Buti za mabao Qatar hizi hapa

Boots Goals Buti za mabao Qatar hizi hapa

Mon, 28 Nov 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Huko Qatar sio tu nchi ndizo zinazopambana kusaka ubingwa wa Kombe la Dunia, bali hata kampuni za watengenezaji wa buti za kuchezea soka zipo kwenye mchuano mkali kwelikweli kuona ni mastaa gani wanaovaa buti za kampuni gani na dizaini gani zinatamba kwenye mikikimikiki hiyo.

Nike na Adidas dizaini zake ndizo zinazoongoza kwa kuvaliwa na mastaa wengi waliopo kwenye fainali hizo za Kombe la Dunia ambazo kwa sasa ipo kwenye hatua ya makundi.

Cristiano Ronaldo ni staa wa Nike, wakati Lionel Messi yeye ni Adidas. Wawili hao kila mmoja amefunga mara moja, tena kwa mikwaju ya penalti, Ureno ilipoichapa Ghana mabao 3-2 na Argentina ilipochapwa na Saudi Arabia 2-1 mtawalia.

Lakini, ni chata gani ya viatu vya mpira inayotamba kwenye viwanja vya Kombe la Dunia huko Qatar?

Mwanaspoti linakumegea uhondo huo wa kampuni inayoongoza kuwa na mastaa wengi wanaovaa viatu vyake kwenye fainali za Kombe la Dunia 2022 huko Qatar, pamoja na dizaini gani iliyohusika kwenye mabao mengi hadi sasa.

Nike ndiyo kampuni yenye mastaa wengi wanaovaa viatu vyao huko Qatar kwenye fainali za Kombe la Dunia, ikimiliki asilimia 49.4. Kuna mastaa 441 wanavaa buti za kampuni hiyo wanakipiga huko kwenye fainali za Qatar.

Adidas yenyewe ina mastaa 311 wanaovaa buti zao kwenye fainali hizo za Qatar ikiwa sawa na asilimia 34.8 ya wakali walipo kwenye mchakamchaka huo wa kusaka ubingwa wa dunia.

Puma, ambao moja ya mastaa wake ni mkali wa Ufaransa, Olivier Giroud inafuatia ikiwa na asilimia 12.1 ya wanasoka waliopo kwenye fainali hizo za Kombe la Dunia 2022 ambao wanavaa viatu vyao.

Mizuno ina mastaa 15 wanaovaa buti zao kwenye fainali hizo za Qatar, ikiwa sawa na asilimia 1.7 ya wachezaji wote. Kitu kinachoshangaza, New Balance ina wachezaji 10, akiwamo mkali wa England, Bukayo Saka na hivyo kuwa na asilimia 1.1 ya wanasoka wote waliopo kwenye fainali za Kombe la Dunia 2022 wanavaa buti za kampuni yao. Under Armour na kampuni ya Mexico, Pirma zenyewe kila moja ina wachezaji wawili tu wanaovaa buti zao kwenye fainali hizo za Qatar ikiwa ni sawa na asilimia 0.2.

Dizaini zinazotamba

Kwenye fainali hizo za Kombe la Dunia 2022 huko Qatar dizaini ya viatu kutoka kwenye kampuni ya Nike inayotamba na yenye wakali wengi ni toleo la Mercurial. Kuna wanasoka 253 wanavaa dizaini hiyo ya viatu na miongoni mwao ni masupastaa Kylian Mbappe na Marcus Rashford.

Dizaini ya Adidas X yenyewe inavaliwa na wanasoka 164, wakati Nike Phantom inavaliwa na wakali 118.

Dizaini ya miaka mingi ya Adidas Predators yenyewe kwa sasa huko kwenye fainali za Qatar inavaliwa na wanasoka 82, wakati ile la Tiempos kuna mastaa 68 wanatinga buti hizo.

Buti za mabao

Je, kwenye fainali hizo za Kombe la Dunia 2022 ni buti gani zinaoongoza kwa kufunga mabao mengi?

Kwenye hili, Adidas inapindua meza mbele ya Nike. Adidas X Speedportal+ buti zake ndiyo hatari zaidi kwenye kutupia mipira nyavuni, ambapo hadi sasa mabao matano yamefungwa na wachezaji wanaovaa dizaini hiyo ya viatu.

Ferran Torres (2), Alvaro Morata (1), Michy Batshuayi (1), na Saleh Al-Shehri (1) ambao wanavaa dizaini hiyo ya viatu, Adidas X Speedportal+. Dizaini inayofuatia ni ya Adidas X Speedportal.1 ambayo imehusika kwenye mabao manne na wafungaji wake ni Mehdi Taremi (2), Dani Olmo (1), na Takuma Asano (1). Dizaini nyingine iliyohusika kwenye mabao manne ni Nike Phantom GT2, ambayo inavaliwa na Gavi (1), Jack Grealish (1), Adrien Rabiot (1) na Davy Klaassen (1). Mabao mengine manne yamefungwa na wachezaji wanaovaa dizaini ya Nike Zoom Mercurial Superfly 9, na wakali wanavaa dizaini hiyo na mabao waliyofunga kwenye mabano Enner Valencia (2), Marcus Rashford (1) na Kylian Mbappe (1).

Mastaa wa England, Saka na Raheem Sterling wenyewe wanavaa New Balance dizaini ya Furon V7 na wenyewe wamefunga mabao matatu katika fainali hizo za Qatar.

Puma dizaini ya Ultra Ultimates yenyewe pia imehusika kwenye mabao matatu, ikiwamo mawili yaliyofungwa na Giroud dhidi ya Australia na bao jingine lilifungwa na Ritsu Doan wa Japan wakati alipowazamisha Ujerumani.

Adidas Predator Edge.1 Low hadi sasa ina mabao mawili na wafungaji wake ni Jude Bellingham na Marcus Asensio. Mchuano bado unaendelea wakati fainali hizo zitakazofika tamati Desemba 18 kwa sasa imefika kwenye mechi za pili hatua ya makundi.

Chanzo: Mwanaspoti