Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Buti za Mo Salah ni shida Liverpool

Mo Salah S Buti za Mo Salah ni shida Liverpool

Fri, 9 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Maswali ni mengi kuhusu nani atakuja kuchukua mikoba ya Mohamed Salah huko Anfield.

Supastaa huyo wa Misri ameandika jina lake katika kurasa tamu za vitabu vya rekodi tangu alipojiunga na Liverpool mwaka 2017, lakini sasa yupo ndani ya miezi 18 ya mwisho ya mkataba wake Anfield.

Kama atabaki au ataondoka mwishoni mwa mkataba wake, wasiwasi unakuja baada ya Kocha Jurgen Klopp kutangaza mwisho wa msimu huu, atang’atuka, hivyo Liverpool watafute mrithi wake.

Kwa kile ambacho Mo Salah amefanya kwenye kikosi hicho cha Liverpool ndicho kinachoibua maswali mengi, ni nani ataweza kwenda kuvaa buti zake huko Anfield.

Kimsingi, Mo Salah ni winga, lakini hilo halijawahi kuwa shida kwake kwenye kutikisa nyavu na kufunga mabao yanayosaidia timu na kumpa tuzo za ufungaji bora mara kadhaa kwenye Ligi Kuu England.

Mo Salah amekuwa na matumizi bora kwelikweli ya mguu wake wa kushoto. Mchezaji mwingine ambaye amekuwa akidaiwa ni mkali kwa mguu wa kushoto na anaweza kuwa mrithi sahihi wa Mo Salah ni winga wa zamani wa Manchester City, Leroy Sane.

Kitu kizuri kuhusu Sane, si mgeni kwenye mikikimikiki ya Ligi Kuu England, akitua Anfield ataendelea tu pale alipoishia alipokuwa Etihad kabla ya kutimkia zake Allianz Arena kuungana na Bayern Munich kwao Ujerumani.

Ukimweka kando Lionel Messi, Mo Salah na Sane ni wachezaji ambao wamekuwa wakitendea haki miguu yao ya kushoto. Lakini, Liverpool inaweza pia kwenda na chaguo la staa wa West Ham United, Jarrod Bowen.

Siku za karibuni, Liverpool ilikuwa ikihusishwa na mpango wa kumsajili Kylian Mbappe.

Lakini, uhakika wa kunasa saini ya mkali huyo wa kimataifa wa Ufaransa umepungua kwa kiasi kikubwa kutokana na mchezaji huyo kuripotiwa atakwenda Real Madrid mwishoni mwa msimu huu.

Awali, Liverpool ilikuwa inahitaji huduma ya mchezaji anayefanana kiuchezaji na Mo Salah kwa maana ya kutafuta anayetumia vyema mguu wa kushoto, lakini hilo likishindikana, hata kwa staa mwenye uhodari wa mguu wa kulia kama Mbappe haitakuwa tatizo.

Kwa Mbappe kuna ugumu kwa sababu anachotaka Mfaransa huyo ni kwenda kutimiza ndoto zake za kwenda kukipiga Bernabeu, kufuata nyavo za mashujaa wake, Cristiano Ronaldo, Zinedine Zidane na Karim Benzema.

Bukayo Saka wa Arsenal ni chaguo jingine la mchezaji mwenye umahiri wa mguu wa kushoto anayeweza kwenda kurithi mikoba ya Mo Salah huko Liverpool.

Lakini, kwa sasa Arsenal nao wamekuwa moja ya timu zenye nguvu kwenye kushindania ubingwa, hivyo Liverpool haitakuwa na nguvu yenye kutisha sana katika kumshawishi Saka ang’oke Emirates kwenda Anfield, licha ya kwamba kufanya hivyo kutamweka kwenye urahisi mkubwa wa kubeba mataji kuliko akiendelea kubaki na The Gunners.

Kuhusu chaguo la mchezaji mwenye mguu wa kulia, Rafael Leao anaweza kuwafaa Liverpool kwenye kusaka mtu wa kuvaa buti za Mo Salah. Staili yake ya uchezaji ya kukokota mpira kuwafuata mabeki ni kitu kinachomfanya afanane na Mo Salah.

Mreno huyo pia ana uwezo wa kufunga mabao na kuasisti, eneo ambalo Mo Salah amekuwa akitendea haki kubwa. Kama Liverpool itafanikiwa kumnasa Leao kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi, basi watakuwa wamemsajili mchezaji huyo akiwa na umri sawa na walivyomchukua Mo Salah kutoka AS Roma kuja Merseyside.

Lakini, kama Liverpool inataka mchezaji wa kushoto, kwa sababu kulia tayari inao wakali wawili matata kabisa, Cody Gakpo na Darwin Nunez, chaguo la mchezaji mwenye mguu wa kushoto linaweza kumhusu zaidi Saka.

Je, watampata? Mikel Arteta atakubali kuachana na silaha yake hiyo inayomfanya atambe Emirates?

Mguu wa kushoto mwingine ambao Liverpool wanaweza kusumbuka kuupata ni wa mkali wa Chelsea, Cole Palmer.

Kama Chelsea itaendelea kucheza kwa kiwango cha hovyo na kumaliza msimu bila ya kukamatia tiketi ya kucheza michuano ya Ulaya, kuna uwezekano mkubwa Liverpool wakamshawishi Palmer na kunasa saini yake.

Palmer ni mchezeshaji zaidi, lakini anaweza pia kufunga mabao. Kingine Palmer atakachokwenda kuwapa Liverpool ni uhakika wa mpigaji penalti. Mchezaji mwingine anayeweza kuwa chaguo sahihi huko Liverpool kwenye kusaka wa kuvaa kiatu cha Mo Salah ni Bryan Mbeumo.

Timu nyingi kwenye Ligi Kuu England zinapiga hesabu za kwenda kumsajili Ivan Toney wa Brentford, lakini Liverpool inapaswa kwenda kwa pacha wake, Mbeumo, kwa sababu ndiye tishio zaidi uwanjani.

Yankuba Minteh ni chaguo jingine linaloweza kufikiriwa na Liverpool. Takwimu za mchezaji huyo si haba sana, akiwa na wastani wa kugusa mipira zaidi ya mara 10 ndani ya boksi la wapinzani.

Kuna kinda mwingine ambaye Liverpool inapaswa kumtolea macho Abdul Fatawu. Kipaji maridhawa kabisa.

Takefusa Kubo amepata mafunzo ya kutosha Barcelona na Real Madrid na uwezo wa miguu yake ni mikubwa kuna kitu itafanya atakapotua zake Anfield.

Mjapani huyo alionyesha kiwango bora sana akiwa Real Sociedad msimu uliopita, alipoweka rekodi za kibabe sana kwenye La Liga, kwa namna alivyokuwa akigusa mpira mara nyingi kwenye boksi la timu pinzani.

Umri wake ndio kwanza miaka 22, hivyo ni staa ambaye atakuwa na muda wa kutosha wa kuja kuitumikia Liverpool itakapofanikiwa kunasa saini yake. Nani atakuja kurithi buti za Mo Salah? Staa huyo yupo kwenye rada za timu kibao za Saudi Arabia.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live