Bunda Queens imetwaa ubingwa wa Ligi Daraja la Kwanza kwa Wanawake Bara (WFDL) baada ya kuichapa Geita Gold bao 1-0 katika mchezo wa fainali ambao umepigwa leo kuanzia saa 9:30 Alasiri Uwanja wa Nyamagana.
Timu hiyo yenye maskani yake wilayani Bunda, Mara imebeba ubingwa huo na kupanda daraja kwenda Ligi Kuu, ikiwa ni miezi michache tu tangu ilipotwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) mwaka jana jijini Mwanza.
Bao la Bunda Queens limefungwa na Bahati Steven dakika ya 11 na kudumu kwa dakika zote 90 za mchezo huo likiwa ni bao lake la tano. Geita Gold imemaliza ya pili na kupanda daraja kwenda Ligi Kuu msimu ujao na kutengeneza historia ya timu ya kwanza ya Wanawake kutoka mkoa wa Geita kucheza ligi hiyo.
Bilo FC ya Mwanza imefanikiwa kukamata nafasi ya tatu ya michuano hiyo baada ya kuwafunga ndugu zao wa Ukerewe Queens kwa bao 1-0 katika mchezo wa mapema ulioanza saa 7:30 mchana.
Michuano hiyo iliyoanza Aprili 13 ikishirikisha timu 14 kutoka Bara imehitimishwa leo katika Uwanja wa Nyamagana, Mwanza huku timu za Mlandizi, Mt. Hanang, TSC na Lengo Queens zikishuka daraja.
Bao alilofunga kwenye fainali hiyo, Bahati Steven wa Bunda Queens ni la tano katika michuano hiyo na kumfanya kuwa kinara wa mabao msimu huu, akifuatiwa na Melkia William na Jamila Selestine (Bunda Queens) na Mary Juma (Ukerewe Queens) ambao wamemaliza na mabao manne kila mmoja.
Kocha wa Bunda Queens, Alley Ibrahim amesema mafanikio hayo ni matunda ya uwekezaji walioufanya wa miaka minne ambapo wamekaa na kikosi chao kwa muda wote huo na kutengeneza muunganiko na timu imara ambayo imetwaa RCL na WFDL.
"Tulijipanga na tulikuja kwa malengo mawili kupanda daraja na kutwaa ubingwa, Tunamshukuru Mungu tumefanikisha yote. Nawapongeza wachezaji wangu na kila mmoja aliyetuunga mkono sasa tunajipanga kwa msimu ujao Ligi Kuu," amesema Ibrahim.
Kutokana na ushindi wa leo, Bunda Queens imevuna Sh 1.1 milioni ambazo ni zawadi kutoka kwa wadau mbalimbali ambao waliahidi kununua kila bao Sh 50,000 hatua ya nusu fainali na Sh 100,000 kwenye fainali akiwamo Mjumbe wa halmashauri kuu ya CCM Taifa, Joyce Mang'o na mfadhili wao, Kambarage Wasira.
"Hawa ni watoto wetu kwa kushirikiana na wadau mbalimbali tumepata Sh 1,160,000 na kuwapa, Mimi ni mlezi wao na nawaahidi nitakuwa nao bega kwa bega wakiwa Ligi Kuu kuhakikisha wanafanya vizuri," amesema Joyce.