Hadi sasa hakuna mchezaji mzawa aliyetingisha usajili kwenye dirisha hili kwa maana ya kuzigonganisha timu kubwa tatu za juu katika kuwania saini yake.
Mara ya mwisho kushuhudia miamba ya soka Tanzania Yanga, Simba na Azam FC ikipigana vikumbo kwa kuwania saini ya mchezaji wa ndani kwa nguvu kabisa ni msimu wa 2020/2021 na mwamba aliyeigonganisha ni huyu Mdigo, Bakari Nondo Mwamnyeto.
Aliingia Yanga ikiwa chini ya nahodha Lamine Moro, hakukuwa na nahodha msaidizi baada ya Juma Abdul kuondoka, hivyo aliyekuwa kocha Msaidizi, Juma Mwambusi na Meneja, Hafidh Saleh walipendekeza jina la Mwamnyeto kuwa Nahodha Msaidizi na alipata kura 16 kati ya 19 za wachezaji. Akawa nahodha wa kuchaguliwa kidemokrasia.
Kiwango cha Lamine kiliyumba, Mwamnyeto akaanza kuvaa kitambaa cha Unahodha “Usinga” na hata Yanga walipoachana na Lamine tayari usinga wa Yanga ulishamzoea.
Akiwa nahodha ameingoza Yanga kutwaa mataji sita kwenye misimu miwili na pia kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Pamoja na mafanikio ya uwanjani Mwamnyeto anabaki kuwa mchezaji ghali Mtanzania ambaye alitingisha dirisha la usajili Tanzania.
Usajili wake Jangwani, ulikutana na maandiko hasi kutoka kwa baadhi ya waandishi na wachambuzi wanaoaminika kuwa na nguvu hapa nchini. Kuna waliodiriki kusema alipaswa kwenda nje ya nchi na si Yanga na kuna waliosema anakwenda kupotea mbele ya Lamine na wengine walimtabiria anguko kubwa la kurejea Coastal Union msimu unaofuata.
Uteuzi wake kuwa nahodha msaidizi ulihojiwa na utaratibu uliotumika ulizua gumzo kwenye vyombo vya habari na kila kitu cha Mwamnyeto kikawa stori kubwa.
Kuna wakati hakuwa sawa, maneno yakawa mengi, na wengi walidhani ndio mwisho wake huku watesi wake wakipata upenyo kutaka kumalizia, lakini alijipanga upya na kurejea kwa nguvu, kasi na maarifa zaidi kuliongoza jahazi la Wanajangwani.
Ahsante nahodha, ahsante kapten wa viwango unayetoa somo nzuri kwa wachezaji wenzako wazawa bila kushika chaki.
Mwamnyeto ana nidhamu, heshima, upendo na utu, zaidi ameshika dini. Mwamnyeto una msemo wako “Kila hatua Dua.” Usiache kumuomba Mwenyezi Mungu katika kila hatua unayoipitia.
Kila la heri katika msimu mpya!
Imeandikwa na Hassan Bumbulumbu (Afisa habari wa zamani wa Young Africans)