Afisa Habari wa Klabu ya Hassan Bumbuli, kupitia Mkutano na waandishi leo Februari 8, 2022 amezitaja takwimu ambazo zinaonesha kuwa na utata katika kuweka usawa kwenye Timu ya Yanga Dhidi ya Wapinzani wao Simba.
Moja ya Takwimu ambayo ameitaja ya kwanza ni Dakika za Nyongeza ambazo hutolewa mwishoni mwa mchezo.
Bumbuli amesema kuwa katika michezo 14 ambayo Klabu ya Young Africans ilicheza kwenye Ligi Kuu msimu huu, walibahatika kuongezewa dakika 34 tu (Jumla) ikiwa na mgawanyiko wa ongezeko la dakika 2, 3 mpaka 5.
Kwenye Michezo 15 ambayo Klabu ya Simba iliyocheza kwenye Ligi Kuu msimu huu, waliongezewa Dakika 75 ikiwa na Mgawanyiko wa Ongezeko la Dakika 4, 5 mpaka 7.
“Tunataka Waamuzi wetu waanze kujitafakari juu ya haya ambayo yamekuwa yakiendelea na yamekuwa mjadala mkubwa sana kwenye Taifa letu, Lakini pia tunataja mamlaka zinazosimamia mpira zichukue hatua juu Ya jambo hili ambalo watu wamewekeza pesa zao.
“Hii imetokana na mlolongo wa matukio ya maamuzi yenye utata ambayo Kwa namna moja au nyingine yananyima haki ya timu zingine na yanatoa manufaa Kwa timu zingine.
“Tunaongoza Ligi hii kwa tofauti ya alama 5 tukiwa na matumaini makubwa yakwamba tuna kikosi imara na tunakwenda kushinda ubingwa msimu huu, pamoja na hayo yote Klabu ya Yanga tunapenda kueleza kwamba haturidhishwi na mwenendo wa baadhi waamuzi wanaocheza michezo ya Ligi kuu,” amesema Bumbuli.