Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino ya Young Africans Hassan Bumbuli amesema Mshambuliaji Ditram Nchimbi, bado ni sehemu ya kikosi cha Young Africans licha ya nje ya kambi, baada ya kupewa ruhusa kufuatia matatizo ya kifamilia.
Uthibitisho huo umetoka baada ya vyombo vya habari kuripoti taarifa za Mshambuliaji huyo kutemwa, kufuatia mkataba wake kuwa mbioni kufikia kikomo mwezi Desemba.
Bumbuli amesema suala la Nchimbi kuanza kuzungumzwa katika vyombo vya habari kuhusu mkataba wake kumalizika, linatokana na kanuni kuruhusu, hivyo Uongozi wa Young Africans haujashtushwa na lolote, lakini ukweli ni kwamba ataendelea kuwa sehemu ya kikosi hadi itakapothibitika anaachwa kwa mapendekezo ya benchi lao la ufundi.
“Ni kweli Ditram Nchimbi mkataba wake unaisha mwezi Ujao tarehe 15, na ndipo dirisha la Usajili dogo litafunguliwa, ndio maana kwa sasa taarifa mbalimbali zinaongea kuhusu yeye sababu kanuni zinamruhusu”
“Kwa sasa yuko nje ya kambi yetu sababu aliomba ruhusa kwenda kwao kutokana na matatizo ya kifamilia, lakini mambo yake yatakapoisha atarejea kambini”
“Tunasubili taarifa ya mwalimu baada ya mchezo dhidi ya Mbeya Kwanza FC, itakayoelezea ni wachezaji gani wa kuachwa na wachezaji gani wa kusajiliwa.” amesema Bumbuli
“Kwa hiyo ripoti ya mwalimu ikionyesha anahitaji kuendelea kubaki na Nchimbi tutakaa nae mezani, lakini ikionyesha hamhitaji basi tutamtakia Kila la kheri.” Amesema Bumbuli.
Tangu kuanza kwa msimu huu 2021/22 Mshambuliaji Ditram Nchimbi hajawahi kuwa sehemu ya kikosi cha Young Africans kilichoshiriki michezo ya Ligi Kuu, huku akiwa chaguo la tatu baada ya Fiston Mayele na Heritier Makambo.