Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bukayo Saka katika nyakati za sahihi za ubora wake

Bukayo Saka Bukayo Saka

Sun, 2 Apr 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Bukayo Saka anajiandaa kuwa mchezaji anayelipwa pesa nyingi zaidi Arsenal atakaposaini mkataba mpya. Winga huyo Mwingereza yupo katika hatua za mwisho kumwaga wino wa kuendelea kubaki Emirates ambapo dili hilo litamfanya awe analipwa Pauni 300,000 kwa wiki. Mkataba wa sasa wa Saka utafika tamati 2024 - ikiwa ni miezi 15 tu imebaki. Mkataba mpya utamfanya aendelee kuvaa uzi wa The Gunners hadi 2028.

Dili hilo jipya litamfanya Saka apate utajiri anaostahili kutokana na kiwango chake bora anachokionyesha huko Arsenal kwa sasa. Saka mwenye umri wa miaka 21, amekuwa mchezaji wa kwanza kufikisha tarakimu mbili kwenye mabao ya kufunga na kuasisti katika Ligi Kuu England msimu huu. Amefunga mara 12 na kuasisti 10.

Lakini, swali linaloulizwa kuhusu Saka ni kwamba atatoboa? Hilo linakuja baada ya kuonekana kama vile kuna gundu kwenye mishahara mikubwa Arsenal. Ni kwamba mchezaji anapolipwa mshahara mkubwa tu Arsenal, anashuka kiwango.

Mwaka 2012, Lukas Podolski alifanywa kuwa mchezaji anayelipwa pesa nyingi zaidi Arsenal wakati alipotua kwenye kikosi hicho akitokea Koln. Winga huyo wa Kijerumani alikuwa analipwa Pauni 157,000 kwa wiki na alionyesha ubora wake kwenye msimu wa kwanza, akifunga mara 16 katika mechi 42 za michuano yote.

Lakini, ghafla kiwango cha Podolski kilianza kushuka na kujikuta akipoteza nafasi katika kikosi hicho chini ya kocha Arsene Wenger msimu wa 2014/15. Podolski alijikuta akitolewa kwa mkopo Inter Milan kabla ya kutimkia Galatasaray jumla mwaka 2015.

Mambo hayakuwa mazuri pia kwa Mesut Ozil baada ya kula dili la pesa ndefu. Mjerumani huyo alisaini mkataba mpya mwaka 2018 uliomshuhudia akilipwa Pauni 350,000 kwa wiki. Kabla ya dili hilo, Ozil alikuwa moto ndani ya uwanja na kuwa mmoja wa mastaa wa Arsenal tishio, lakini baada ya dili tu kila kitu kilibadilika kiasi cha kutolewa bure kabisa kikosini. Ozil aliondoshwa na kocha Mikel Arteta katika msimu wa 2018/19 akiwa amefunga mabao sita na kuasisti mara tatu.

Arsenal haikujifunza juu ya gundu la mishahara mikubwa kwa mastaa wake, wakampa dili tamu pia straika Pierre Emerick-Aubameyang baada ya kuwasaidia kubeba Kombe la FA mwaka 2020. Aubameyang alikuwa analipwa Pauni 250,000 kwa wiki akiwazidi Thomas Partey, Willian na Alexandre Lacazette. Mambo yakaibuka na kuwa mabaya tena kwa mkali huyo, akapoteza nafasi kikosini na kujikuta akitolewa bure kabisa kwenda Barcelona.

Kuondoka kwa Aubameyang kulimfanya Gabriel Jesus kuwa mchezaji anayelipwa mshahara mkubwa zaidi kwenye kikosi cha Arsenal. Na hivi unavyosoma hapa, staa huyo wa Kibrazili ndiyo kwanza anarejea uwanjani kujaribu kujiweka sawa baada ya kuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu kufuatia kuumia kwenye fainali za Kombe la Dunia 2022 huko Qatar. Kabla ya hapo, Jesus alikuwa kwenye kiwango bora kabisa, lakini sasa anajikongoja kurejea kwenye ubora wake.

Kwa sasa, Saka yupo kwenye kiwango bora kabisa cha soka lake na Arsenal wanaamua kumpa mkataba mpya wa kumpandishia mshahara na kumfanya kuwa mchezaji anayelipwa pesa nyingi Emirates. Atabaki salama? Atapona kwenye lile jinamizi linalowakumba mastaa wa Arsenal wanapopewa mikataba ya pesa nyingi? Ngoja tuone.

Chanzo: Mwanaspoti