Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bukayo Saka aibua hofu nyingine Arsenal

Bukayo Saka Injury Bukayo Saka aibua hofu nyingine Arsenal

Tue, 17 Sep 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Arsenal jasho linawatoka wakihofu wachezaji wenye majeraha kuongezeka kwenye kikosi chao baada ya Bukayo Saka kuumia na kulazimika kutolewa kwenye mechi ya ushindi wa bao 1-0 katika North London derby dhidi ya Tottenham Hotspur.

Saka alipotoka nafasi yake aliingia Ethan Nwaneri kwenye dakika 10 za mwisho za mchezo huo, lakini kitendo cha winga wao Saka alipoonekana akitikisa kichwa alipokuwa chini baada ya kuumia, ndicho kinachowapa wasiwasi mashabiki.

Arsenal tayari haina mastaa Mikel Merino, Martin Odegaard, Riccardo Calafiori, Takehiro Tomiyasu na Oleksandr Zinchenko kutokana na kuwa majeruhi. Na sasa mashabiki wa Arsenal wanaanza kupata wasiwasi wa kumpoteza Saka huku wakiwa na mechi ngumu ya ugenini kukipiga na Atalanta kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya keshokutwa Alhamisi na baada ya hapo itakwenda kukipiga na Manchester City kwenye Ligi Kuu England.

Katika mitandao ya kijamii, shabiki mmoja aliandika: “Sikupenda vile Saka alivyotikisa kichwa chake - tafadhali isiwe siriazi.”

Shabiki mwingine aliongeza: “Natumai kutolewa kwa Saka ilikuwa ni wasiwasi tu hakikuwa kitu siriazi...”.

Na shabiki wa tatu kwa hasira aliandika: “Majeraha ya Saka ni kitu cha mwisho kabisa tunachokihitaji!”

Shabiki wa nne aliposti: “Siwezi kudanganya, majeraha ya Saka yanatia presha.”

Kwenye mchezo wa Spurs, Arsenal ilifunga kwa mpira wa kutenga, ambapo beki Gabriel aliunganisha kwa kichwa kwenye ushindi wa 1-0. Nahodha Odegaard anasumbuliwa na maumivu ya enka, wakati Merino aliumia bega na Calafiori na Zinchenko wana maumivu ya miguu huku Tomiyasu anasumbuliwa na maumivu ya goti.

Chanzo: Mwanaspoti