Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bruno sasa njia nyeupe Ihefu

Bruno Gomes Text Friend Bruno sasa njia nyeupe Ihefu

Fri, 8 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Viongozi wa Ihefu wameanza mazungumzo kimyakimya ya kumnyatia aliyekuwa kiungo wa Singida Fountain Gate Mbrazili, Bruno Gomes aliyevunja mkataba wake hivi karibuni na timu hiyo kwa ajili ya kujiunga nayo msimu ujao wa mashindano mbalimbali.

Nyota huyo aliyeitumikia Singida kwa misimu miwili akitoka klabu ya Jacobinense EC ya kwao Brazili, aliachana na kikosi hicho baada ya kufikia makubaliano ya pande mbili jambo ambalo viongozi wa Ihefu wameanza hesabu za kunasa saini yake.

Taarifa za kuaminika kutoka ndani ya Ihefu zilizotua Mwanaspoti, zimethibitisha ni kweli mazungumzo yanaendelea ya kumshawishi kusaini kwa ajili ya msimu ujao, wakiamini atakuwa chachu ya mafanikio kutokana uhusiano mzuri na wachezaji waliopo.

“Ni kweli viongozi wamekuwa katika mawasiliano naye ya kumshawishi kuingia naye mkataba kwa ajili ya msimu ujao, Bruno ni mchezaji mzuri tunayeamini kama atajiunga nasi basi atakuwa na msaada mkubwa kikosini kwetu,” kilisema chanzo chetu.

Akizungumzia suala hilo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Ihefu, Olebile Sikwane alisema kwa sasa hawajaanza mipango ya msimu ujao kwa sababu akili zao ni kuhakikisha timu hiyo inamaliza msimu vizuri katika michezo iliyosalia na wala sio vinginevyo.

“Siwezi kuzungumza jambo hilo kwa sasa kwani sio muda muafaka kwake, hivyo tuachane nalo hadi wakati utakapofikia,” alisema.

Kwa upande wa Bruno alisema, kwa sasa hajafanya uamuzi juu ya timu atakayoichezea msimu ujao kwani anahitaji kupumzika kwanza.

Endapo dili hilo litakamilishwa basi nyota huyo ataungana na wakali wengine waliowahi kucheza pamoja Singida Fountain Gate ambao ni Aboubakar Khomeiny, Kelvin Nashon, Duke Abuya, Marouf Tchakei, Joash Onyango na Elvis Rupia.

Msimu uliopita ndio ulikuwa bora kwa Bruno, akifunga jumla ya mabao 10 ya Ligi Kuu Bara na kuzivutia Simba na Yanga, tofauti na msimu huu mambo yamekuwa magumu kwa kuandamwa na majeraha akifunga bao moja tu.

Chanzo: Mwanaspoti