Kiungo Mshambuliaji wa Singida Big Stars, Bruno Gomes amesema tuzo ya mchezaji bora wa Januari aliyoipata imemuongezea motisha zaidi ya kuipambania timu yake ili ifanye vizuri.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, nyota huyo kutoka Brazil alisema tuzo hiyo ni maalumu kwa timu yao nzima kwani bila ya ushirikiano mkubwa anaoupata kutoka kwao asingeweza kufanikisha jambo hilo.
“Kikubwa ni mshikamano uliopo baina yangu na wachezaji wenzangu, kiukweli najisikia furaha sana lakini jambo la msingi na ahadi yangu kwa mashabiki ni kupambana zaidi ya hapa,” alisema Bruno.
Kwa upande wa Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Singida, Muhibu Kanu alisema kiwango alichokionyesha mchezaji wao amestahili huku akibainisha malengo yao kama klabu ni kuona wanazidi kupiga hatua.
Bruno amechukua tuzo hiyo baada ya kuwashinda, Ibrahim Mkoko wa Namungo FC anayekumbukwa kwa kupiga ‘hat-trick’ kwenye mchezo dhidi ya KMC na Mkongomani, Henock Mayala wa Polisi Tanzania.
Mbali na Bruno pia kocha wake Mholanzi, Hans Van Pluijm amechukua tuzo ya kocha bora wa Januari baada ya kuwashinda Roberto Oliveira ‘Robertinho’ wa Simba na Nasreddine Nabi wa Yanga.