Tukio la staa wa Singida Big Stars, Bruno Gomes, la kwenda kwenye bechi la Yanga kabla ya kuanza kwa mechi yao ya Ligi Kuu Bara juzi limetingisha mitandao ya kijamii na kuzua sintofahamu kubwa lakini kumbe ishu iko hivi.
Tuanze hapa, Bruno kabla ya mchezo kuanza alimfuata kocha wa makipa wa Yanga, Milton Nienov ambaye ni raia mwenzake wa Brazil kisha wakakumbatiana lakini hakuishia hapo akarudi kuwasalimia makocha na wachezaji wote waliokuwa kwenye benchi la Wanajangwani, hatua ambayo iliwashtua mashabiki na kuanza kumshangilia kwa nguvu uwanjani.
Kumbe kulikuwa na ishu ya wachezaji wa timu zote mbili kwenda kuwasabahi watu ambao wanatokea katika nchi moja.
Winga wa Yanga, Jesus Moloko yeye alimfuata mshambuliaji mwenzake Mkongomani Fancy Kazadi aliyekuwa kwenye benchi la Singida Big Stars kusalimiana naye.
Lakini sintofahamu zaidi ikaendelea baada ya Bruno kwenda kwenye akaunti yake ya Instagram baada ya mechi na kuandika maneno yaliyofananishwa na kauli mbiu ya Yanga 'Daima kusonga mbele! Mungu ni mwema' akiambatanisha na picha yake akimshukuru Mungu akiwa amepiga magoti.
Matukio hayo mawili yamewashtua mashabiki wa Yanga wanaoheshimu ubora wa kiungo huyo huku watani wao wakianza kusonya wakidhani kuwa watani wao na ukaribu wao na Singida Big Stars basi imeisha hiyo.
Mwanaspoti linajua kuwa hatua hiyo imewashtua sio tu mashabiki wa Yanga bali hata vigogo wa Yanga waliokuwa uwanjani na hata kuona alichoandika wakibaki kucheka na kuulizana huku wakigoma kusema chochote.
Rais wa Yanga Injinia Hersi Said aligoma kabisa kuzungumzia matukio hayo akiishia kucheka lakini Mwanaspoti linafahamu kuwa kuna idadi kubwa ya vigogo wa Yanga walishawishika na kiwango cha Mbrazil huyo.
Hata hivyo, usajili wa Bruno kwenda Yanga Mwanaspoti linakuhakikishia kuwa mabosi wa Yanga wamemuachia kocha wao Nasreddine Nabi kuamua na kutoa baraka zake tu ili matajiri wao wa GSM waingie kazini.
"Mnataka Gomes? Hilo sio suala gumu ni uamuzi wa kocha tu (Nabi) akisema basi atatua Jangwani, hilo hata yeye Nabi anajua, tumemuachia atuambie kiufundi kama anamfaa au vinginevyo," alisema bosi mmoja wa juu wa Yanga.
Juzi kocha msaidizi wa Yanga, Cedric Kaze akizungumzia hatua hiyo ya Bruno alisema kiungo huyo mshambuliaji aliwafuata kwenye benchi hilo kwa ajili ya kumsalimia kocha wao wa makipa Nienov.