Kiungo mshambuliaji wa Singida Big Stars, Bruno Gomes raia wa Brazil ameamua kukata mzizi wa fitna kwa mashabiki wa chama lake baada ya kuhusishwa kwenye tetesi za kujiunga na Yanga msimu ujao, huku akisema waliongea mambo ya mechi siyo usajili.
Bruno kwenye mechi dhidi ya Yanga ambayo Singida BS ilifungwa mabao 2-0 (Alhamisi) mchezaji huyo alisalimiana na benchi zima la ufundi la Yanga kabla mchezo haujaanza na mchezo ulivyomalizika alionekana kuzungumza kitu sambamba na kocha wa makipa wa Yanga, Milton Nienov na kiungo timu hiyo Stephen Aziz Ki.
Kiungo huyu pia baada ya kutoka uwanjani aliweka picha kwenye ukurasa wake wa mtandao wa Instagram akiandika; "Daima kusonga mbele Mungu ni Mwema."
Kauli hiyo ni kama vile imechochea uvumi wa yeye kwenda Yanga na Mwanaspoti lilipomtafuta alisema; "Hapana yale ni maneno ya kawaida kama ambayo huwa naandika siku zote."
"Rafiki yangu hili ni jambo la kawaida kusalimia watu kwani hata mechi zingine huwa nafanya hivyo, kweli nilikuwa naongea nao baada ya mchezo lakini tulikuwa tunazungumza kuhusu mchezo wote kiujumla na siyo ishu ya usajili,"alisema Bruno.
Bruno wakati anajiunga na Singida BS alisaini mkataba wa miaka miwili lakini baada ya kuonyesha kiwango kizuri aliongezewa mkataba mwingine wa miaka mitatu itakayomfanya aendelee kusalia katika timu hiyo.
Kiungo huyo mwenye mabao tisa kwenye Ligi Kuu Bara anatajwa kuwa mmoja kati ya wachezaji mahiri kwenye ligi msimu huu hadi sasa.