Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bruno, Pepe kukumbana na Rungu la FIFA

Bruno Anda Pepe Pic Bruno, Pepe kukumbana na Rungu la FIFA

Tue, 13 Dec 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Mastaa wa timu ya taifa Ureno, Bruno Fernandes na Pepe huenda wakapewa adhabu na Shirikisho la Soka Kimataifa (Fifa) baada ya kumchana wazi mwamuzi Fecundo Tello, aliyechezesha mchezo wao dhidi ya Morocco, kwenye mechi ya robo fainali ya Kombe la Dunia.

Morocco iliichapa Ureno bao 1-0 kwenye Uwanja wa Al Thumana na kuiondosha mashindanoni na kuwa timu ya kwanza ya Afrika kutinga nusu fainali ya Kombe la Dunia huko Qatar.

Lakini nyota anayekipiga Porto, Pepe amesema mwamuzi huyo raia wa Argentina hakupaswa kuchezesha mchezo wao baada ya taifa lake linaloongozwa na Lionel Messi kutinga nusu fainali.

Bruno na Pepe wanaamini kuna mipango ilifanyika ili mwamuzi huyo achezeshe mechi yao ili kuwapa faida Argentina waibuke mabingwa wa Kombe la Dunia mwaka huu.

Beki huyo wa zamani wa Real Madrid alisema Argetina itapewa tu ubingwa wa Kombe la Dunia mbele ya waandishi wa habari baada ya mtanange wao kumalizika Ureno ikishindwa kufurukuta mbele ya Morocco licha kuongezwa dakika nane za majeruhi.

“Inashangaza sana kuona mwamuzi kutoka Argentina anachezesha mechi yetu, kwa kile nilichoona kwenye mechi ya Argentina, naona kabisa Argentina ikipewa ubingwa,” alisema Pepe.

Naye nyota anayekipiga Manchester United, Bruno alimuunga mkono mchezaji mwenzake Pepe akisisitiza: “Sijui kama hiyo Argentina itapewa ubingwa, sijali, kinachoshangaza zaidi refa kutoka Argentina amechezesha mechi yetu, imeonekana wazi kuna njama zimepangwa juu yetu.”

Sasa baada ya kauli hizo FIFA itafuatilia kwa makini kuhusu madai ya Bruno na Pepe kabla kuchukua hatua dhidi yao na huenda wakapewa adhabu.

Vile vile, kipa wa Argentina, Emiliano Martinez huenda naye akapewa adhabu na Fifa baada ya kumkebehi mwamuzi Antonio Lahoz aliyecheza mechi yao ya robo fainali dhidi ya Uholanzi kwa kumuita mjinga. Imeelezwa kipa huyo anaweza akaukosa mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Dunia dhidi ya Croatia kesho.

Wakati huo huo, Cristiano Ronaldo aliondoka uwanjani akibubujikwa na machozi baada ya kuondoshwa mashindanoni huku taarifa zikiripoti huenda fainali za Kombe la Dunia za mwaka huu ndio zikawa za mwisho kwa upande wake.

Chanzo: Mwanaspoti