Afya ya nyota wa Singida Big Stars, Mbrazili Bruno Gomes inaendelea kuimarika baada ya kupata majeraha ya kifundo cha mguu wakati akiwa mazoezini na kikosi hicho mkoani Singida.
Bruno mwenye mabao tisa katika Ligi Kuu Bara, akiwa ndiye kinara wa timu hiyo alipata majeraha hayo baada ya kuumizwa na mchezaji wenzake, Hamad Waziri ‘Kuku’.
Daktari wa timu hiyo, Shaaban Shija aliliambia Mwanaspoti kuwa “Anaendelea na matibabu vizuri na huenda akakaa nje kwa muda wa wiki moja, aliumia vibaya na kama Bruno asingelegeza mguu, basi tungeweza kuongea mengine maana angevunjika,” alisema Dk Shija, huku kocha wa kikosi hicho, Hans Pluijm alisema baada ya tukio hilo kutokea alikaa chini na Hamad na kumweleza jambo analopaswa kuzingatia zaidi ni kujali afya za wenzake.
“Hajaonyesha kitendo cha kiuungwana kwa mchezaji mwenzake lakini inatokea hilo kwa sababu sio mara ya kwanza, kila mmoja wetu ana haki ya kumlinda wenzake na kuepusha majeraha yasiyokuwa na ulazima.”
Hamad alijiunga na Singida kupitia dirisha dogo lililofungwa Januari 15 mwaka huu akitokea Mbeya City na ni mmoja ya mabeki wanaosifika kwa kutumia nguvu awapo uwanjani au kwenye mazoezi. Singida inacheza na Mtibwa mechi ijayo.