Kiungo wa Singida Fountain Gate ya Singida, Bruno Gomes leo Machi 4, 2024 ametangaza kusitisha mkataba wake na timu hiyo baada ya kuitumikia kwa muda wa mwaka mmoja na miezi sita.
Katika taarifa yake aliyoitoa leo, kiungo huyo ametaja sababu ya kuvunja mkataba huo kuwa ni klabu kukiuka mkataba wake.
"Leo nina habari muhimu ya kushiriki nanyi. Baada ya kutafakari kwa kina na majadiliano, tumefikia uamuzi mgumu, lakini tunaamini ni bora kwa pande zote zinazohusuka.
"Ningependa kuwajulisha kwamba kumekuwa na uvunjaji wa mkataba kwa upande mmoja kutoka kwa klabu na kwa bahati mbaya hii imesababisha kumalizika kwa uhusiano wangu na klabu hiyo.
"Uamuzi huu haukuwa rahisi, lakini ulifanyika kwa nia ya kuhakikisha tunaweza kuendelea mbele kwa njia ambayo ni chanya na yenye ujenzi kwa wote," alisema Bruno.
Kiungo huyo Mbrazil aliyejiunga na Singida Fountain Gate mwaka 2022 akitokea Jacobinense ya Brazil alisema bado ataendelea kuipa heshima klabu hiyo.
"Ingawa mkataba wetu umefikia kikomo, jua kwamba upendo na heshima niliyonayo kwenu itabaki milele. Kamwe sitasahau mchango mlionao kwangu kama mchezaji na mtu.
"Asante kwa kushiriki shauku yenu ya soka nami. Natumai tutaendelea kudumisha uhusiano huu maalum hata kama njia zetu zitachukua muelekeo tofauti," alisema Gomes.