Mabosi wa Azam FC wakishirikiana na Benchi la Ufundi wameanza kutembeza panga kwa kufyeka baadhi ya wachezaji, ili kutoa nafasi ya usajili wa msimu mpya wa 2023/24.
Azam inayoshika nafasi ya tatu kwa sasa kwenye msimamo wa ligi na ikiwa tayari ipo Fainali ya Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ ikitarajiwa kuvaana na Yanga, Jumatatu ijayo kwenye Uwanja wa Mkwakwani, jijini Tanga inataka kufyeka nyota waliopo ili kuingiza mastaa wengine wapya.
Taarifa kutoka Chamazi zinaeleza kuwa tayari mabosi wa Azam FC wameshaweka rehani baadhi ya majina ya watakaofyekwa kikosini kwa ajili ya maandalizi ya msimu ujao, wakiwamo Yahya Zayd, Bruce Kangwa, Ismail Kada na Cleophace Mkandala.
Zayd, Kada na Mkandala hawajawa kwenye kikosi cha kwanza kiasi cha kufanya kuleta ushindani kwa wachezaji wanaoanza ndani ya timu hiyo.
Upande wa Kangwa, licha ya kuwa mchezaji wa kikosi cha kwanza lakini inaelezwa mabosi wanaona ni wakati wa kumtoa ili walete damu change kwenye kikosi chao.
Kutolewa kwa Kangwa kuna mvutano kwa mabosi wa timu kwani wengine wanataka aendelee kuwepo kwani licha ya kusajili mabeki wa kushoto kama Edward Manyama akiwa kwenye kiwango kizuri lakini ameshindwa kucheza mbele ya Kangwa.
Hivyo, licha ya Kangwa yupo kwenye hatari ya kukatwa lakini bado kuna mvutano kwa mabosi wa timu hiyo.
Chanzo kimoja kutoka ndani ya timu hiyo kimesema; “Kangwa ndiye mchezaji pekee ambaye mabosi wanavutana hadi sasa kutokana na kile ambacho amekuwa akikionyesha tofauti na hao wengine.”
Hata hivyo alipotafutwa Msemaji wa Azam FC Hasheem Ibwe kuzungumzia panga hilo amesema kwa sasa akili zao ni kumalizia mechi mbili za Ligi Kuu na ile ya Fainali ya ASFC dhidi ya Young Africans.