Tuliwalipia zile tatu Simba’. Ni kauli ya shabiki wa kutupwa wa Yanga Andrew Ngonyani ‘Brother K’ akielezea furaha ya ushindi wa jana akisema waliwalipia watani zao na kurejesha furaha kwenye nchi.
Yanga jana ikicheza kwa ubora wake kwenye uwanja wa Taifa Dar es Salaam iliinyuka TP Mazembe mabao 3-1 ikiwa ni mchezo wa pili katika michuano ya kombe la Shirikisho Afrika.
Kabla ya Yanga kufanya kweli, ilitanguliwa mchezo wa klabu bingwa Afrika ambapo watani zao Simba walikunjwa mabao 3-0 Jumamosi dhidi ya Raja Casablanca ikiwa ni kipigo cha pili mfululizo kwa Wekundu hao.
Brother K ambaye ni shabiki mkubwa wa Yanga amesema jana licha ya kurejesha furaha kwa Taifa, lakini ilikuwa ni kuwalipia kisasi watani zao waliopoteza mchezo wakiwa nyumbani.
Amesema Yanga ya sasa haikamatiki akibainisha kuwa kuwafunga Mazembe timu kubwa Afrika ni kuonesha uimara wa timu hiyo inayotetea ubingwa wake wa ligi kuu kwa msimu wa pili mfululizo.
“Mpira ulipigwa, mabao yakafungwa, hii ndio Yanga timu ya Wananchi, tulichofanya ni kurejesha furaha kwa watanzania kwa sababu wale wenzetu walituaibisha hivyo amani ikapotea ila tulilipa kisasi,” amesema Mchekeshaji huyo.
Mvunja mbavu huyo ameongeza kuwa pamoja na kiwango cha wachezaji wote kwa kila mmoja kutimiza wajibu wake, lakini kazi aliyoifanya Fiston Mayele ilimkosha sana.
“Yanga ndio bingwa kwa mara nyingine Ligi Kuu hilo halina upinzani, ila niwapongeze vijana wote kwa kazi nzuri jana japokuwa Mayele alikuwa moto sana angalia lile bao la tatu,” ametamba komedi huyo.