Klabu ya Yanga imetangaza kuachana na aliyekuwa kiungo mshambuliaji wake, Bernard Morrison raia wa Ghana baada ya mkataba wake wa kuitumikia klabu hiyo kufika ukingoni.
Taarifa iliyotolewa na Yanga imeelza;
Uongozi wa Young Africans Sports Club unapenda kuwajulisha Wanachama na Mashabiki wa Yanga kuwa mchezaji Bernard Morrison amemaliza muda wake wa ndani ya Klabu hiyo.
Morrison alijiunga na Yanga mwaka 2022 kwa mkataba wa mwaka mmoja akiwa kama mchezaji huru.
Uongozi wa Yanga unapenda kumshukuru Morrison kwa mchango wake ndani ya Klabu katika kipindi cha mwaka mmoja, akichangia mafanikio makubwa ya kubeba Mataji matatu na kuifikisha timu kwneye mchezo wa Fainali ya Kombe la Shirikisho la CAF.
Itakumbukwa kuwa, Morrison alijiunga na Yanga kwa Mara ya kwanza katika dirisha dogo la usajili mwaka 2019 akiwa mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba wake na AS Vita Club ya Congo.
Aliitumikia Yanga kwa miezi 6 pekee kisha kujiunga na Simba ambapo aliibua kasheshe Yanga wakidai ni mchezaji wao na amesaini mkataba wa miaka miwili, sakata lake lilikwe sa TFF kisha likafika CAS lakini iliamriwa kuwa mkataba wake na Yanga ulikuwa na mapungufu hivyo aliendelea kucheza Simba.
Baada ya kuichezea Simba kwa mafanikio makubwa ndani ya miaka miwili, alimaliza mkataba wake kisha akarejea tena Yanga lakini tabia zake za utukutu na uvivu wa mazoezi magumu ndio zinatajwa kama kigezo cha mabosi wa Jangwani kugoma kumuongezea mkataba mwingine.