Klabu ya Yanga imemtambulisha mshambuliaji mpya, Kennedy Musonda kutoka katika klabu ya Power Dynamos ya nchini Zambia ambaye amesajiliwa rasmi na klabu hiyo.
Huu unakuwa usajili wa pili wa Yanga katika dirisha dogo baada ya kiungo fundi Mudathiri Yahya aliyesajiliwa klabuni hapo wiki iliyopita kufuatia akiwa amemaliza mkataba wake na Azam FC.
Musonda aliyekuwa kwenye rada za vigogo wengi wa soka la Afrika, alichagua Yanga baada ya ushawishi mkubwa alioupata kutoka kwa Rais wa Yanga, Eng Hersi Said.
"Kulikuwa na ofa nyingi sana mezani kutoka timu tofauti tofauti kubwa barani Afrika, lakini kitu kimoja ambacho nilikuwa nina uhakika nacho baada ya kuongea na Rais Yanga, nilijua nimefanya uamuzi sahihi wa kujiunga na Timu kubwa na bora zaidi" alisema Musonda.
Musonda anatarajiwa kutua Tanzania kesho Jumamosi, Januari 14, 2023, saa 8:45 mchana kwa shirika la ndege la Kenya akitokea Zambia na kujiunga na kikosi cha Yanga kwa ajili ya maandalizi ya mechi za Ligi na Hatua ya Makundi ya Kombe la Shirikisho la CAF.
Ikumbukwe kuwa Msemaji wa Yanga Sc, Ally Kamwe hivi karibuni alinukuliwa akisema kuwa wanahitaji kusajili wachezaji wawili tu wa kimataifa kwenye dirisha hili dogo ambalo linatarajia kufungwa Usiku wa Januari 15, 2023, ambao ni mshambuliaji na beki wa kati.
Taarifa kutoka Zambia ni kwamba Musonda ambaye amepewa dili la maana na timu hiyo ya Jangwani na sasa atatakiwa kufanya kazi haswa ili kuwapa imani mashabiki wa timu hiyo.
Dynamos imechukua fedha nzuri katika dili hilo kiasi kisichopungua Tsh milioni 150 kutoka kwa Yanga ambao wamenunua mkataba wa staa huyo uliokuwa umebaki.
Pia, Musonda naye amechukua kiasi kama hicho ili kusaini dili la miaka miwili na Yanga huku mshahara wake ukiwa Tsh milioni 11 kwa mwezi akiwa kati ya wachezaji wanaolipwa ghali zaidi kwenye Ligi Kuu Bara kwa sasa.
Mshambuliaji huyo mwenye miaka 29, metoka kwenye timu yake akiwa ndiye kinara wa mabao kwenye Ligi Kuu ya Zambia msimu huu, ambapo hadi sasa ameshafunga mabao 11.
Mshambuliaji huyo ambaye aidha watacheza pamoja au mmoja ataanzia nje kati yake na Fiston Mayele mwenye mabao 14 kwenye ligi msimu huu, aliwahi pia kuzichezea Lusaka Dynamos, Zanaco na Green Eagles kwa mafanikio makubwa.