Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bravo Yanga hii ya Gamondi imeenda

Gamondi X Yanga Somo Bravo Yanga hii ya Gamondi imeenda

Mon, 2 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Hatimaye ule mzimu uliokuwa unaitesa Yanga kwa miaka 25 mfululizo ya kushindwa kutinga makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, umetupiliwa mbali baada ya juzi usiku wababe hao wa Tanzania kuifumua Al Merrikh ya Sudan kwa bao 1-0 na kutinga hatua hiyo kwa ushindi wa jumla wa mabao 3-0.

Awali, Yanga ilipata ushindi wa 2-0 ikiwa ugenini jijini Kigali, Rwanda ambapo Wasudan walipatumia kama uwanja wa nyumbani kutokana na wasiwasi wa usalama katika taifa hilo linaloandamwa na machafuko ya kisiasa.

Mara ya mwisho kwa Yanga kucheza hatua hiyo ilikuwa mwaka 1998 mara baada ya michuano hiyo kubadilishwa kutoka Klabu Bingwa Afrika hadi kuwa Ligi ya Mabingwa na shukrani za pekee zinapaswa kumuendea straika chipukizi, Clement Mzize aliyepachika mabao mawili kati ya matatu yaliyoivusha.

Katika mechi ya juzi, Yanga ilionekana kuzibiwa mianya kwa muda mrefu na Al Merrikh, ambayo hata hivyo haikuweza kulikaribia lango la Wananchi na hivyo kumfanya kipa Djigui Diarra kukosa kazi ya kufanya kwa muda mwingi wa mchezo. Kujilinda kwa kutumia idadi kubwa ya wachezaji kuliwasaidia kufukia kila aina ya shimo na kuwadhibiti nyota wa Jangwani hususani aliyekuwa na siku yake, Stephane Aziz KI, lakini dakika ya 66 waliruhusu bao la kichwa kutoka kwa Mzize aliyemalizia krosi ya beki wa kushoto, Joyce Lomalisa aliyepokewa pasi ndefu ya kiungo Khalid Aucho aliyeng’ara kwenye mechi hiyo.

Yanga imetinga makundi ikiungana na wababe wengine, ikisubiri droo ya kujua itapangwa na timu zipi kabla ya kuanza msako wa heshima kwenye michuano hiyo ambayo kwa kutinga tu makundi tayari imejihakikisha kuvuna kitita cha Dola 700,000 (zaidi ya Sh1.8 bilioni).

Haikuwa kazi rahisi kwa Yanga kufikia mafanikio hayo, lakini inaonyesha hesabu za uongozi wa klabu hiyo chini ya Rais Injinia Hersi Saidi na wenzake imelipa, kwani rekodi zinaonyesha wakati timu hiyo ikicheza makundi mwaka 1998, rais huyo alikuwa kidato cha kwanza yaani bwana mdogo asiyejua kama angekuja kuifikisha klabu hiyo hapo kwa sasa.

WASUDAN WALIBANA

Kipindi cha kwanza kilikuwa kigumu kwa Yanga kupenya ukuta wa wageni wao waliokuwa wanatumia mfumo wa 4-2-3-1 ambao uliwapa ubora mkubwa ukawafanya wenyeji wao kushindwa kupenya safu ya ulinzi.

Yanga iliuanza mchezo kwa tempo ya chini sana ikiwasubiria Merrikh ijiachie ili iwaingize kwenye mtego, lakini hatua hiyo haikuwa rahisi kwani wageni nao walikuwa imara kwa nidhamu ya mchezo.

Kocha Miguel Gamondi aliingia uwanjani na wachezaji karibu wote waliocheza mechi ya Kigali, isipokuwa alimuanzisha Clement Mzize na Pacome Zouzoua nje kabla ya kuwaingiza kipindi cha pili na kuwabadilisha Wasudani soka kisha kuwazima kwa bao 1-0 lililowapa furaha mashabiki wa Jangwani.

MOLOKO MH!

Kama kuna mchezaji aliyeinyima Yanga mabao ya mapema kwenye mechi ya juzi basi ni Jesus Moloko, kwani hakuwa kwenye ubora aliozoeleka na alikuwa akipoteza mipira mara nyingi na kuishia kucheza faulo au kuangushwa na mabeki wa Sudan.

Endapo winga huyo kutoka DR Congo angekuwa kwenye kiwango bora angeisaidia vizuri timu yake kupata mabao katika kipindi cha kwanza kutokana kupewa mipira mingi lakini pasi zake za mwisho zilipotea.

Inakokwenda katika makundi Yanga inatakiwa kuliboresha eneo hilo kwani hatua hiyo watakutana na watu bora zaidi ambao sio rahisi kukupa nafasi nyingi kama ambazo anahitaji Moloko kuweza kutengeneza nafasi nzuri za mabao.

BAO LATOKA NJE

Baada ya kumalizika kwa dakika 45 za kwanza kocha Gamondi alianza kipindi cha pili na mabadiliko akimtoa mshambuliaji Kennedy Musonda nafasi yake ikichukuliwa na mwenzake Clement Mzize ambaye ndiye aliyekuja kufunga bao la kwanza.

Mzize mara baada ya kuingia aliutumbukiza mpira wavuni kwa kichwa katika dakika ya 47 akimalizia krosi ya Maxi Nzengeli lakini mwamuzi wa pili msaidizi Urbain Ndong kutoka Gabon kibendera chake kilikuwa juu kwa maelezo kwamba alipiga krosi mpira ukiwa umetoka.

Mzize alikuja kufunga bao la ushindi jana kwa njia ile ile ya kichwa akitumia krosi ya beki wake wa kushoto Joyce Lomalisa Mutambala.

Ukiacha kuingia kwa Mzize pia mabadiliko ya kumtoa Aziz KI na kuingia Pacome Zouzoua pia yaliiongezea ubunifu Yanga na kuanza kuongeza kasi ya kuwatawanya mabeki wa Merrikh.

Mzize anazidi kuimarika taratibu ndani ya kikosi cha Yanga anapata muda wa kucheza na anautumia vizuri bila kujali ameanza au ametokea benchi, yuko kwenye hesabu sahihi ndani ya kichwa cha Gamondi akilipa imani ambayo anapewa na makocha wake

MECHI YA MBINU

Licha ya matokeo kuwa ni bao 1-0 lililowabeba Yanga, lakini mchezo wa juzi kifupi ulitawaliwa na mbinu zaidi, huku kila timu ikionekana kumsoma mwenzake, kiasi ilikuwa ngumu kubaini timu ipi ingetoka na ushindi au kupotea mchezo huo.

Yanga ilicheza kwa akili ya kulinda ushindi wa ugenini, wakati wenzao wa Al Merrikh walikuwa na mbinu za kusaka angalau wapate bao la kuwarudisha mchezoni.

Mara baada ya kubaini mbinu za kupata bao la kuongoza imekuwa ngumu ndipo makocha walifanya mabadiliko, yaliyoinufaisha Yanga, kwani Al Merrikh ilionekana kuchoka na kucheza rafu mara nyingi na kuishia kulalamika kwa mwamuzi ambaye alionekana hana masihara kwa mechi ya juzi.

Wasudani walikosa ubunifu wa kuipenya ngome ya Yanga kwani katika dakika 90 walifanikiwa kupiga mashuti matatu pekee ambayo nayo hayakulenga lango, moja likipigwa kipindi cha kwanza dakika ya 32 na beki Salaheldin Nemer kipindi cha kwanza na mengine mawili yakipigwa na Mussa Alli.

YANGA IFANYE NINI?

Inapoingia makundi Yanga inakuwa ni kati ya timu 16 zilizopenya hatua hiyo na sasa inapaswa kufunga mkanda kwelikweli kama inataka kuvuka hatua hiyo salama na kwenda robo fainali kwa mara ya kwanza kwenye mfumo wa sasa wa Ligi ya Mabingwa.

Yanga inaungana na Pyramids, Al Ahly (Misri), Jwaneng Galaxy (Botswana), TP Mazembe (DR Congo), Petro Atletico (Angola), Etoile du Sahel, Esparence (Tunisia), Wydad Athletic (Morocco), Mamelodi Sundowns, Medeama (Ghana) na jana ilitarajiwa kufahamika timu tano za mwisho za kutinga hatua hiyo kabla ya kufanyika droo baadaye mwezi huu na mechi za hatua hiyo kuja kupigwa mwishoni mwa Novemba.

Kwa sasa Yanga inatakiwa kufanya tathimini kubwa ya kikosi chao na hasa eneo lao la ushambuliaji ambalo bado halina makali sana kuweza kuhimili presha ya mechi kubwa kama hizo ambazo zinafuata.

AZAM COMPLEX HAUTOSHI

Nje ya mchezo huo kama kuna mashabiki wanaukumbuka Uwanja wa Benjamin Mkapa basi ni mashabiki wa Yanga, timu yao iko kwenye moto na wana morali kubwa ya kuja kwenye mechi zao lakini uwanja haukubaliani na idadi yao.

Yanga imekuwa ikishinda vizuri ndani ya Azam Complex pengine kuliko hata Uwanja wa Benjamin Mkapa lakini bado kuna mashabiki wengi wanalazimika kuukosa mchezo huo kutokana na nafasi ndogo, kwani unaingiza watu wasiozidi 10,000, wakati Kwa Mkapa unabeba watazamaji 60,000.

Yanga mbali na kaundika rekodi ya kutinga makundi kwa mara ya pili ikiwa ni baada ya miaka 25 iliyopita, imeandika historia pia ya kuitoa kwa mara ya kwanza timu kutoka Sudan, na pia kuishinda Al Merrikh ambayo kwenye mechi nne za awali walizowahi kukutana ilikuwa haijashinda zaidi ya sare mbili za nyumbani na kupoteza ugenini, lakini safari hii imeshinda nje ndani na kuvuna Dola 700,000 (zaidi ya Sh1.8 bilioni).

WASIKIE MAKOCHA

Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi alisemam alifurahishwa na kiwango cha timu yake akisema kwasasa wanajipanga kwa hatua ya makundi wakitaka kwenda kushindana na sio kushiriki.

“Nilisema mwanzo kwamba itakuwa mechi ngumu lakini tumefanikiwa kushinda tena, mabadiliko ambayo tuliyafanya kipindi cha pili yalitupa nguvu ya kupata bao la ushindi tayari tumeshaingia kwenye hatua ya makundi hii ni hatua moja tunatakiwa sasa kujipanga kwenda kushindana na sio kushiriki,” alisema Gamondi, huku Osama Nabih wa Al Merrikh alisema wamekubali matokeo ya kutolewa na Yanga, licha ya awali walijipanga kushindana kwa kupindua meza, ila alikiri kikosi hicho kiliathirika na kukosa mechi nyingi za ushindani.

“Ukiangalia mechi hizi mbili utaona tofauti kubwa tulikutana na timu ambayo iko juu yetu wanacheza kwa haraka kwa kuwa wameiva kwa kucheza kwao mechi za ligi na hizi za Ligi ya Mabingwa, timu yangu haikuwa na ubora mkubwa kuweza kushindana kwa nguvu tunalazimika kukubaliana na hali halisi,”alisema Nabih raia wa Misri.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: