Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba SC, Salim Abdallah Try Again’ ametamba sababu ya ufunguzi wa michuano ya Ligi ya Afrika unafanyika Tanzania kwa sababu timu yao ni kubwa.
Salim amesema mafanikio ambayo Simba SC imeyapata ndio yamewapa heshima na Tanzania kuteuliwa kuwa mwenyeji wa mechi ya ufunguzi.
“Simba SC ni kubwa, mashabiki wa Simba wanapenda mpira, Watanzania wanapenda mpira,” Salim alisema.
Mwenyekiti huyo pia alisema kikosi chao kinajiandaa vyema na kitakwenda Zambia kucheza mechi dhidi ya Power Dynamos kwa tahadhari.
Ule ulikuwa mchezo wa kirafiki, mchezo wa kirafiki na mchezo wa mashindano ni vitu viwili tofauti, tunaiangalia Power Dynamos katika jicho kali sana, tunakwenda na tahadhari zote,” alisema kiongozi huyo.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally, alisema mashabiki wanaokwenda kuishangilia timu yao katika mechi hiyo ya ugenini wataondoka nchini Septemba 13, mwaka huu na utaratibu wa safari unatolewa katika ofisi ya klabu yao.
Ahmed amesema gharama za usafiri wa kwenda na kurudi kwa kila shabiki ni Sh. 200,000 na mwisho wa kupokea fedha hizo ni Septemba 10, mwaka huu.
Katika hatua nyingine, Simba inatarajia kucheza mechi ya kirafiki leo dhidi ya timu ambayo haijatangazwa huku pia ikijiandaa kuelekea Kenya kuweka kambi ya muda mfupi kabla ya kwenda Zambia.