Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bosi Tabora United abwaga manyanga

Thabit Kandoroooo Mtendaji Mkuu wa Tabora United, Thabit Kandoro

Wed, 27 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Mtendaji Mkuu wa Tabora United, Thabit Kandoro amejiuzulu nafasi hiyo siku chache baada ya kumtimua aliyekuwa kocha mkuu wa timu hiyo, Goran Kopunovic.

Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya timu hiyo kimeliambia Mwanaspoti kuwa Kandoro amejiengua nafasi hiyo kutokana na kukabiliwa na matatizo ya kifamilia.

Wakati baadhi ya viongozi waking'oka, inasemekana makocha wawili, Denis Goavec, kocha mkuu na Masoud Djuma, waliotua kuchukua nafasi ya Goran bado hawajamalizana na uongozi wa timu hiyo.

"Ni kweli Kandoro kajiweka pembeni kutokana na matatizo yake binafsi na tayari kawasilisha barua ya kujiweka pembeni, kinachosubiriwa ni majibu kutoka kwa viongozi," alisema.

"Leo mapema alikuwepo kwenye mazoezi yaliyofanywa na timu lakini kilichowazi ni kwamba barua ya kujiweka pembeni imepokewa na viongozi majibu yatatolewa," kilisema chanzo hicho.

Kuhusu kocha mkuu, chanzo hicho kilisema ni kweli kocha hajasaini mkataba lakini ni suala la muda kwani kilichobaki ni kufanya hivyo tu kwasababu mazungumzo baina yao yamekamilika.

"Kocha kasimamia mazoezi jana na leo, suala la kutokusaini ni la muda tu, mazungumzo yamekwenda vizuri na makubaliano yao yapo vizuri," kilisema chanzo hicho ambacho hakikutaka jina lake litajwe gazetini.

Alipotafutwa Ofisa Habari wa Tabora United, Christina Mwagala alisema suala la Kandoro litatolewa taarifa muda wowote kuanzia sasa.

"Sitaki kuzungumza mambo mengi, kama suala hilo lipo mtaona taarifa kutoka ndani ya uongozi tusubiri muda ukifika watafanya hivyo," alisema Mwagala.

Tabora United ambayo ilipanda Ligi Kuu Bara msimu huu ikitokea Championship, iko hatarini kurudi ilikotoka, ikiwa na pointi 21, pointi moja tu juu ya mstari wa kushuka daraja huku timu iliyo chini yake ya JKT Tanzania ikiwa na pointi 20 na mechi moja mkononi. Chini ya timu hizo mbili, mkiani, ipo Mtibwa Sugar yenye pointi 16 na mechi moja mkononi.

Chanzo: Mwanaspoti