Wakati Simba ikiwa kwenye mchakato wa kumtangaza kocha wao mpya mara baada ya kuachana na Mbrazili, Roberto Oliveira ‘Robertinho’, uongozi wa Simba umewatoa hofu mashabiki wa timu hiyo kwa kuweka wazi kuwa kikosi chao kiko kwenye mikono salama.
Simba juzi Jumanne ilitangaza kufikia makubaliano ya pande mbili ya kuachana na aliyekuwa kocha wao mkuu Robertinho kwa kile kilichoelezwa kiwango kibovu cha timu hiyo hususani kipigo cha mabao 5-1 walichokipata kutoka kwa watani zao wa jadi, Yanga.
Pamoja na taarifa hiyo, Simba pia walitangaza kikosi hicho kwa sasa kitakuwa chini ya kocha wao wa makipa, Daniel Cadena na kusaidiwa na Selemani Matola.
Makocha hao wanatarajiwa kuiongoza Simba katika mchezo wa Ligi Kuu Bara utakaochezwa leo Alhamisi dhidi ya Namungo kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Akizungumza nasi, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, alisema: “Tunaelekea katika mchezo mgumu dhidi ya Namungo ambapo kikosi kipo chini ya kocha Daniel Cadena ambaye amekabidhiwa jukumu la kuiongoza timu yetu kwa kipindi hiki.
“Niwatoe hofu mashabiki wa Simba kuwa, huyu ni kocha mwenye wasifu na uwezo mkubwa, hivyo wakati huu tukitafuta kocha wa kudumu tuwe na imani kuwa Simba yetu ipo katika mikono salama.”