Mwenyekiti wa zamani wa Klabu ya Simba, Ismail Aden Rage amesema kuwa kiungo mshambuliaji wa watani zao, Klabu ya Yanga, Pacome Zouzoua ni mtu na nusu kwani amekuwa akionyesha kiwango kizuri kadri siku zinavyokwenda.
Rage amesema hayo kufuatia matokeo mazuri waliyopata Yanga juzi, Februari 24, 2024 kwa kuifunga CR Belouizdad bao 4-0 na kutinga hatua ya robo fainali ya CAFCL wakiwa na mchezo mmoja mkononi, na kuvunja rekodi yao ya miaka zaidi ya 52 iliyopita kufika hatua hiyo.
Katika mchezo huo, Pacome alitengeneza nafasi tano kati ya 10 ambazo Yanga walitengeneza ambapo kwenye nafasi hizo, nafasi moja ilikuwa bao ambalo alifunga kennedy Musonda.
"Pacome amenifurahisha sana na ningekuwa na namba ya Kocha wa Timu ya Taifa ya Ivory Coast ningemkosoa nikamwambia umefanya makossa, unaangalia straikers wako wanaotoka Ulaya lakini wanaotoka Afrika unawadharau.
"Kwa kweli ningempa maneno yake, Pacome anafaa kuwekwa kwenye kikosi cha Timu ya taifa ya Ivory Coast.
"Ni mchezaji ambaye kama unakumbuka Simba alivyopigwa bao 5, yeye ndiye alikuwa akitengeneza mipango yote mapaka magoli yanaingia kirahisi. Ni mchezaji mzuri sana," amesema Rage.