Wakati Simba wakiwa njiani kurejea nchini wakitokea Uturuki kwenye maandalizi ya msimu ujao wa 2023/24, taarifa njema ni kuhusiana na kiungo wao mpya, Fabrice Ngoma ambaye unaambiwa anawapa jeuri mabosi na mashabiki wa timu hiyo kutokana na aina yake ya uchezaji katika eneo la kiungo.
Ngoma ambaye amepita katika klabu kubwa Afrika ikiwemo AS Vita ya DR Congo, Raja Casablanca (Morocco) na Al Hilal (Sudan), kwa sasa ni mali ya Simba kutokana na kusaini mkataba hivi karibuni.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally amesema kuwa, aina ya uchezaji wa Ngoma ni wa kipekee na ndani ya kikosi chao utawaongezea ubunifu mkubwa uliokosekana katika maeneo ambayo anacheza, hivyo wanatarajia makubwa zaidi kutoka kwake.
“Ngoma ana staili yake ya pekee ya kucheza soka, uchezaji wake umekosekana ndani ya Simba kwa maana ya kuwa kiungo wa chini kisha akawa na uwezo mzuri pia wa kushambulia na kufunga, hiyo kwetu haikuwepo, hivyo kwa ujio wake niwaambie tu wanasimba watafurahia zaidi.
“Sio tu Ngoma, wachezaji wote ambao tumewasajili ni wachezaji bora ambao watatufanya watupeleke katika nchi ya ahadi kwa kuwa naamini kila ambaye tumemsajili kipindi hiki ni mchezaji bora na ana uwezo mkubwa sana,” alisema kiongozi huyo.
Tayari kikosi cha Simba kimeshavunja kambi yake nchini Uturuki baada ya kumaliza maandalizi kuelekea msimu mpya na wachezaji, benchi la udfundi pamoja na viongozi waliokuwa wamekwenda na timu wameanza safari ya kurejea nchini.
Jumapili, Agosti 6, SImba watawaalika Power Dynamo FC ya Zambia kwa ajili ya mchezo wa kirafiki kwenye Tamasha la Simba Day.