Kwa mujibu wa taarifa za ndani kutoka Manchester United, tajiri wa timu hiyo, Sir Jim Ratcliffe amewaambia wafanyakazi wao wanatakiwa kurudi ofisini kufanya kazi kwa ufanisi ama wakishindwa watafute kazi nyingine ya kufanya.
Inaelezwa Ratcliffe anataka kuboresha timu hiyo kuanzia levo za chini hadi juu ndani na nje ya uwanja ili kuongeza ufanisi na kupata matokeo chanya.
Man United imekuwa ikipitia kipindi kigumu hususani katika mechi hizo za mwisho wa msimu na mchezo uliopita ilipokea kichapo cha mabao 4-0 kutoka kwa Crystal Palace.
Licha ya maono yake makubwa ya kutaka Man United iondoke katika hali yake ya sasa na kurudi enzi za zamani, tajiri huyu anaona wafanyakazi wa timu hiyo wanaofanya kazi za nje ya uwanja, hawafanyi vile anavyohitaji na amewatumia ujumbe anafikiria kufuta utaratibu wa kufanyia kazi nyumbani ambao upo sasa.
Kwa mujibu wa tovuti ya Dail Mail, katika ofisi zilizopo ndani ya Old Trafford eneo ni dogo, hivyo baadhi ya wafanyakazi wamepelekwa kwenye uwanja wa mazoezi wa Carrington na wengine wameruhusiwa kufanyia kazi nyumbani.
Lakini Ratcliffe ameonyesha kukerwa na utendaji kazi wa nyumbani na ripoti inaonyesha wamepunguza uwajibikaji kwa asilimia 20.
Kwa sababu hiyo amewatumia email za maelekezo wanatakiwa wote warudi na kufanyia kazi ofisini akiamini hiyo itasaidia kuongeza ufanisi na ushirikiano na kwa mujibu wa ripoti, wafanyakazi wasiotaka kurudi ofisini wameambiwa watafute kazi sehemu nyingine.
Baada ya Mail, kuwatafuta viongozi wa Man United kuzungumzia agizo hilo walikataa kuongea chochote.
Baadhi ya wafanyakazi wameonyesha kuchukizwa na agizo hilo wakiona ni kama mihemko kwa sababu eneo la kufanyia kazi ni dogo, hivyo wanashangaa wakirudi watakaaje ofisini.
Hii sio mara ya kwanza kwa Ratcliffe kuonyesha kuchukizwa na hali ya utendaji kazi wa wafanyakazi wa timu hiyo, kuna wakati alipotembelea Old Trafford na Carrington alisema hajaridhishwa na hali ya mazingira ya malazi kwa timu za vijana na akatoa onyo kwa wahusika.
DILI LA GREENWOOD
Wakati huo huo inaelezwa mshambuliaji wa timu hiyo aliye kwa mkopo Getafe anasakwa na timu kibao nje na ndani ya England.
Greenwood, 22, ameonyesha kiwango bora akiwa na Getafe msimu huu na anacheza kwa mkopo akifunga mabao 10 na kutoa asisti sita katika mechi 32 za michuano yote.
Kutokana na kiwango chake Getafe imeonyesha nia ya kutaka kuendelea kuwa naye lakini Man United kipaumbele chao ni kumuuza.
Kiwango chake ndani ya Hispania msimu huu kimezivuta timu nyingi Ulaya ikiwamo Barcelona, Juventus, Atletico Madrid na Lazio zilizoanza kuhusishwa naye tangu dirisha lililopita na sasa kwa mujibu wa tovuti ya The Telegraph, timu mbili za England zinamtaka ingawa hazijawekwa wazi.
Man United ina matumaini ya kupata zaidi ya Pauni 40 milioni kwa mauzo ya Greenwood ambayo itawasaidia katika harakati za kufanya usajili dirisha lijalo.
Greenwood aliyejiunga na Getafe Septemba mwaka jana na Rais wa Getafe, Angel Torres alipoulizwa juu ya uwezekano wa kumbakisha alisema: “Kama ingekuwa ni uamuzi wa mchezaji mwenyewe, wazazi wake na sisi basi nina uhakika angebakia lakini hili suala lipo kwa Man United na kwa taarifa ambayo tupo nayo baada ya Mkurugenzi wetu wa michezo kwenda kukutana nao ni kwamba kama kuna timu itawasilisha ofa nzuri basi watamuuza, kwa sababu hawezi tena kubaki kwao.”
“Inatakiwa tusubiri hadi mwisho wa mwezi ujao ili kuwa na jibu sahihi lakini nafahamu kwamba familia na mchezaji mwenyewe wana furaha sana ya kuendelea kuwa hapa.”