Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bomu lipo lwa Mayele na Diarra

Mayele X Diarra Bomu lipo lwa Mayele na Diarra

Sun, 18 Jun 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kama kuna kazi ngumu kwenye mchezo wa Soka, basi ni kutengeneza timu. Tuko kwenye zama ambazo kumpata mtu kama Djigui Diarra sio mchezo. Tuko kwenye zama ambazo kumpata Mshambuliaji kama Fiston Mayele ni Shughuli pevu. Makocha Bora wapo wengi.

Ni uwezo wako tu. Ni juhudi zako tu kuwatafuta. Kutengeneza timu bora, unahitaji watu wawili bora karibu kwenye kila nafasi uwanjani. Kuitengeneza timu bora, unahitaji kuwa na watu bora karibu 30. Sio jambo la Kitoto. Ukishakuwa na timu bora, Kocha analeta mbinu tu za ushindi.

Kutengeneza Benchi la Ufundi bora kwa mpira wa Kiafrika sio zaidi ya watu Watano. Nimeiona Taarifa ya Kocha Nasreddine Nabi kuondoka Jangwani. Huu sio Msiba. Ni Taarifa yenye faida kwa pande zote mbili. Sio Taarifa iliyonistua. Sio Taarifa iliyonishangaza.

Siku Djigui Diarra na Fiston Mayele wakiondoka, huu sasa unapaswa kuwa msiba mzito Jangwani. Najua ubora wa Nabi, najua umuhimu wake kwa Yanga lakini Yanga inaweza kuwa bora zaidi bila yeye.

Kazi kubwa kwa Yanga kwa sasa ni kuhakikisha Wachezaji wake wote muhimu wanasalia kikosini. Zipo tetesi za Mayele kuondoka. Ziko tetesi za Diarra kuondoka Jangwani! Hapo ndipo Bomu lilipo.

Kama Yanga watawabakisha Wachezaji wao muhimu, Ujenzi wa benchi la ufundi sio jambo gumu sana. Klabu Simba wakati wanachukuwa Ubingwa mara nne mfululizo miaka ya hivi karibuni wakiwa na kina Luiz Miquessone, Clatous Chota Chama, walikuwa na wastani wa kubadili Kocha kila msimu lakini Simba waliendelea kushinda Ubingwa.

Wananchi,suala la Kocha sio jambo kubwa sana ukishakuwa na wachezaji bora kikosini. Alipoondoka Kocha Pep Guardiola pale FC Barcelona baada ya miaka minne ya mafanikio, Barcelona haikuyumba. Alikuja Kocha Tito Vilanova akatusua. Alikuja Luis Enrique Martínez baadaye na kuendeleza Bakora. Kinachodhoofisha timu nyingi duniani,ni kuondoka Kwa Wachezaji muhimu sio Kocha.

Bado Yanga wananafasi ya kufanya vizuri klabu Bingwa Afrika. Bado Yanga wana nafasi ya kuendelea kukua. Nabi amefanikiwa sana Soka la ndani. Kutwaa Mataji mawili ya Ligi Kuu na lile la Azam Sports Federation, sio kazi ndogo lakini Nabi ameshindwa kwenye Klabu Bingwa. Kwa timu aliyokuwa nayo msimu huu, Nabi alitakiwa kwenda hata Nusu Fainali ya Klabu Bingwa Afrika. Ni rahisi kwa Mashabiki wa Yanga kujipoza na Fainali ya Shirikisho Afrika lakini, hilo halikuwa lengo mama la Klabu ya Yanga.

Kocha Nabi kwa mara ya pili mfululizo ameshindwa kufuzu kwenye makundi ya Klabu Bingwa Afrika. Kuondoka kwake kunatoa mwanya wa Kocha mwingine kuja kuipeleka timu mbele zaidi. Amekuwa mzuri sana wa Soka la nyumbani kama zama za Kocha Hans van der Pluijm.

Ndoto za Yanga kuapata ufalme wa Afrika, haziwezi kutimia kupitia Kombe la Shirikisho. Zinahitaji mtu mwenye uwezo wa kuwavusha ndani ya Klabu Bingwa Afrika. Timu nyingi Afrika zimepungua kiwango. Al Ahly ni Mabingwa kwa mara nyingine wa Afrika lakini msimu huu walikuwa unga sana!

Bado Mamelodi Sundowns sio wale tunaowajua. Kama Yanga wanapata hata Wachezaji watatu tu wa maana na kuwalinda Wachezaji wao bora wa msimu huu wasiondoke, Kocha mpya hatokuwa na kazi ngumu msimu ujao. Ukishakuwa na Wachezaji bora, mtihani wa Kocha sio mkubwa. Kocha anakuja kuleta mbinu tu.

Kupata Wachezaji wazuri ni kazi kubwa kuliko Kocha. Nabi amewakuta Yanga wakiwa na makombe 27. Maana yake nini? Ni rahisi tu. Yanga wanaweza kutwaa ubingwa na Kocha mwingine bila shaka yoyote. Vipi kuhusiana na Kimataifa? Jibu ni kuwa Nabi kawafikisha hatua ambayo hawajawahi kufika. Je, wanaweza kusonga mbele bila yeye? Jibu ni rahisi tu. NDIYO.

Kocha Nabi msimu huu alipaswa kuwapa Yanga Ubingwa kabisa wa Kombe la Shirikisho. Kila kitu kilikuwa kwenye mikono yake na kwa sababu hakufanikiwa hilo, Wananchi watahitaji mtu mwingine mwenye historia na Kombe hilo kukamilisha ndoto hiyo. Vipi kuhusiana na Klabu Bingwa? Nabi alishindwa kabisa!

Kwa mara ya pili mfululizo ameishia hatua za awali tu. Nini Yanga wakifanye? Ni rahisi mno. Kwanza ni kuzuia Wachezaji wao muhimu wasiondoke.

Pili ni kusajili wachezaji walau watatu wa Kikosi cha kwanza na kuleta Kocha mwenye Historia na Kombe lolote la Afrika. Kocha Nabi amesaidia kuongeza Standadi ya Yanga, ni muda wa kuleta Kocha mwingine atakayewapa makombe. Ukishakuwa na timu bora, kazi ya Kocha inakuwa rahisi. Yanga wanahitaji zaidi kuisuka timu kuliko kumlilia Kocha Nabi.

Yanga kiasili ni timu inayoshambulia kwa kutumia mawinga lakini kikosi hiki kimejaa Wanariadha! Yanga wanahitaji Winga kama yule Kipre JR wa Azam FC sio mwanariadha.

Yanga ni lazima wapate mtu wa kuziba nafasi ya Feisal Salum, pale kikosini kwao hayupo. Wanahitaji kupata mtu mwenye ubora kama wa Clatous Chota Chama eneo lile. Ni muhimu sana kupata kiungo mbunifu. Nadhani sasa ni muda wa kuamua kuwatumia Djuma Shabaan na Joyce Lomalisa kwenye maeneo yao asili au kuachana nao. Yanga wanahitaji Beki wa kati Kisiki, yule Doumbia ni kama 'Tetrasaklini'. Leo rangi nyekundu, kesho nyeusi.

Huwezi Kutwaa ubingwa wa Afrika kwa kubahatisha. Linahitajika Dude kama Pascal Wawa wa zama zile. Sioni sababu ya Yanga kumlilia Nabi, hapa alipowafikisha ni Robo ya safari. Wanahitaji mtu mwingine wa kuwapeleka nchi ya ahadi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live