Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bomu linalopikwa Yanga, litakufa jitu tena

Hersi Yanga Gamondiz Bomu linalopikwa Yanga, litakufa jitu tena

Tue, 25 Jun 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Yanga imeanza kusuka safu imara yenye lengo la kucheza fainali za Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao. Wanachowauliza wapinzani wao ni kwamba; “nyie hamuogopi?”

Gumzo kubwa likiwa ni usajili wa mastaa wapya kutoka kwa wapinzani wake, Azam na Simba pamoja na ujio wa vitu vipya kutoka nje ya nchi.  

Yanga inataka kuboresha idara zote tatu za kikosi chao ambapo kuna sura tatu mpya huenda zikashtua zaidi ndani ya kikosi cha mabingwa hao kwa msimu ujao.

BOKA KWENYE UKUTA Mwanaspoti limejiridhisha kwamba beki Mkongomani Chadrack Boka atakuwa ndani ya mziki wa Yanga msimu ujao baada ya kukamilisha dili la miaka miwili akitokea FC Lupopo ya kwao DR Congo. Ingawa lolote linaweza kutokea mazoezini lakini makubaliano ni kwamba anakwenda moja kwa moja kikosi cha kwanza.

Ujio wa Boka una maana kwamba golini Yanga itakuwa na kipa Djigui Diarra, kulia akianza Yao Akouassi, mabeki wa kati wakiwa nahodha Dickson Job na Ibrahim Hamad ‘Bacca’, wakati kule kushoto atakuwa Boka akichukua nafasi ya Mkongomani mwenzake Lomalisa Mutambala ambaye mkataba wake umemalizika na  hajaongezewa sababu kubwa ikitajwa kwamba anataka masilahi makubwa ambayo hayaendani na nafasi pamoja na mchango kikosini. Lomalisa anatajwa kutimkia Arabuni.

Yanga imemalizana pia na kipa wa Ihefu, Abubakari Khomeny ambaye atasaidiana na Diarra.

CHAMA NDANI Lengo la Yanga ni kuhakikisha Clatous Chama anavaa jezi akitokea Msimbazi. Mpaka sasa Mwanaspoti linajua ameshakabidhiwa mkataba wa mwaka mmoja na anao mkononi. Yanga wanataka asimame kwenye kiungo cha juu.

Chama anatajwa kusaini mkataba wa mwaka mmoja na Yanga akitokea Simba alikomaliza mkataba, kama mambo yako hivyo mabingwa hao watakuwa wameongeza mtu mbunifu mwingine atakatayeimarisha eneo hilo haswa kutokana na uzoefu wake kwenye michuano yote.

Hebu angalia chini, Yanga ikianza na viungo wawili wakabaji Khalid Aucho, Mudathir Yahya na juu yao wakiwa Chama, Pacome Zouzoua, na Stephanie Aziz KI huku nje akisubiri Maxi Nzengeli. Aucho alinukuliwa hivi karibuni kuwa moja ya ndoto ni kucheza timu moja na Chama kwani anaamini kitakuwa kiungo bora zaidi kuwahi kutokea.

Kocha wa Yanga Miguel Gamondi anaweza pia kuamua kuanza na mmoja kati ya Chama au Pacome kisha mmoja kati ya hao akianzia benchi kama atataka kuanza na Maxi ambaye ni mchezaji muhimu anayetembea eneo kubwa uwanjani kutokana na nguvu yake ya kujua kubadilika wakati timu ikiwa na mpira na wakati ikiwa haina mpira.

DUBE MBELE Wikiendi iliyopita Dube alionekana Morogoro kwenye mchezo wa hisani wa mastaa wa Yanga wakichangia matibabu ya mama na mtoto, akifunga bao la tatu.

Dube anamalizia sakata lake na klabu ya Azam na tayari ameshawaingizia Sh500Milioni kununua sehemu ya mkataba wake uliosalia. 

Inafahamika kuwa kuna uwezekano akatua Yanga na ameshapewa mkataba wa miaka miwili na anaishi kwenye jumba moja maeneo ya Salasala Jijini Dar es Salaam chini ya ulinzi mkali aliowekewa na watu walioko karibu na Yanga.

Ameweka ulinzi huo ili asishawishiwe na Simba kwa namna yoyote ile. Yanga wanamtegemea kwenye safu yao ya mabao msimu ujao, wanahisi anaweza kuwa mrithi sahihi wa Fiston Mayele.

Dube hajaharibika mwili wake, licha ya kukaa nje muda mrefu akiwa sawasawa kitu ambacho anaonekana atakikosa ni kuwa fiti na hilo pia litamalizwa kwenye maandalizi ya msimu.

Dube kama ataanza nje kutakuwa na watu wawili wa kumsaidia Joseph Guede na Clement Mzize ambao nao ubora wao unazidi kwenda juu. Ingawa kuna habari za chinichini kwamba Yanga wanaweza kufanya uamuzi mgumu wa kuachana na Guede kama hesabu zao zitakaa sawa wakapata straika mzawa mwenye uwezo wa kutupia.

MAONI YA MAKOCHA Kocha wa zamani wa Simba, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ licha ya kushtuka kusikia uwezekano wa Chama kwenda Yanga, alisema endapo hilo litatimia linaweza kuleta shida kubwa kwa timu pinzani kwani kikosi cha mabingwa hao kitaongeza ugumu kwenye safu yao ya ushambuliaji.

“Muda unavyosogea Chama anazidi kwenda mwisho lakini haina maana hataweza kuisaidia Yanga. Tatizo ninaloliona hapa ni kwamba mchezaji bora anakwenda kuunganika na wengine bora hili litakuwa tatizo kwa timu pinzani,” alisema Robertinho ambaye alipoteza kazi baada ya Yanga kumpiga 5-1.

“Nadhani unakumbuka safu yao ya kiungo iliovyokuwa bora msimu uliomalizika, walikuwa na watu wabunifu sana eneo hilo kama yule Pacome,Aziz na Maxi, anapokwenda na Chama itakuwa ngumu zaidi itategemea na hesabu za kocha wao.

“Kuhusu Dube namkumbuka ni mshambuliaji mzuri, unajua ubora wake mkubwa ni kwamba anajua kufunga na kukimbia sio lazima atokee kati kama mshambuliaji makali yake anaweza kuyaonyesha hata akitokea pembeni, nadhani itakuwa timu yenye ujazo mkubwa.”

Kocha wa zamani wa Yanga na Azam FC, George Lwandamina alisema endapo mastaa hao watakamilisha kwenda Yanga itakuwa na kikosi bora ambacho kitamfanya kocha kuwa na deni kubwa la kuifikisha mbali kimataifa na kuonyesha inataka kuendelea kutetea mataji ya ndani.

“Ni mabingwa msimu uliomalizika, kama wamemchukua Chama nadhani wanaonyesha wanataka kitu kikubwa zaidi, Clatous (Chama) ni kijana wangu alianza kuwa bora akiwa chini yangu ni mchezaji mbunifu zaidi kama akikutana na yule kutoka Ivory Coast jezi namba 26 hawa wote ni wabunifu na hawatulii inakuwa shida kutuliza safu ya aina hiyo,” alisema Lwandamina ambaye alirejea Zesco.

“Dube naye nilifanya naye kazi Azam ni mchezaji bora sikuwa na bahati naye kubwa sana kutokana na majeraha yake lakini alipokuwa fiti unaona nguvu imerejea. Kwa timu ambayo wanayo Yanga kama atakwenda huko naona kutakuwa na kazi nzito hasa kama nyuma yake atacheza yule Aziz KI ni mzuri sana wa kutoa pasi za kufunga.”

Chanzo: www.tanzaniaweb.live