Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Boli walisukuma huku a.k.a ziliwabeba vilevile

Canavarooo (1).jpeg Boli walisukuma huku a.k.a ziliwabeba vilevile

Sat, 11 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Huenda usiamini, lakini ndivyo ukweli ulivyo. Mashabiki wa soka wa zamani wanapoyasikia majina ya utani wa nyota wa soka wa sasa wanacheka kwa dharau. Unajua kwanini?

Majina ya utani kwa wachezaji wa sasa hayanogi sana kama ilivyokuwa miaka ya nyuma ambapo a.k.a zilisisimua kwelikweli.

Utamu zaidi ni kwamba baadhi ya a.k.a za nyota wa zamani zilikuwa zinaendana na uhalisi wa vipaji halisi vya wachezaji hao, tofauti na ilivyo sasa, mchezaji anajiita au kuitwa Messi, Neymar au Mbappe kama sio Haaland, lakini kile wanachokionyesha uwanjani ni tofauti na ukubwa wa majina hayo.

Pia, kuna wakati a.k.a za wachezaji wa sasa zimekuwa za kawaida mno kiasi cha kushindwa kuwapa msisimko mashabiki, kwa mfano tu fikiria mtu anapolisikia jina kama la John Bocco ‘Adebayor’ ama Mzamiru Yassin ‘Kiungo Punda’ au Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ ama Zimbwe Jr’ utasisimka vipi mbele ya majina ya utani na vidume vya zamani?

Angalau kidogo majina ya utani ya Jonas Mkude ‘Nungu Nungu’, Ali Nassor ‘Ufudu’, ama walivyokuwa wakiitwa Ame Ali ‘Zungu’ ama Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Haruna Moshi ‘Boban’ ambao uwanjani yaliendana na uhalisia wa soka lao na hata matendo, japo bado hayakusimua sana.

Mwanaspoti linakukumbushia baadhi ya majina ya bandia a.k.a zilizokuwa zikisusumua na kuendana na uhalisia wa soka la waliopachikwa majina hayo ambapo hadi leo bado yanakumbukwa.

Celestine Mbunga ‘Sikinde’ Winga machachari wa zamani wa Majimaji, Yanga na Taifa Stars alibatizwa jina la Sikinde kwa madai ya aina ya uchezaji wake ambapo wakati akiwapiga chenga mabeki alikuwa kama mtu anayecheza miondoko ya Sikinde.

Miondoko hiyo inatumiwa na bendi maarufu na Mabingwa wa Muziki wa Dansi, DDC Mlimani Park Orchestra ‘Wana Sikinde Ngoma ya Ukae’. Sunday Manara ‘Computer’

Nyota huyo wa zamani wa Yanga, Pan Africans na Taifa Stars aliyekuwa wa kwanza kucheza soka la kulipwa barani Ulaya, Manara alibatizwa jina hilo hata chombo hicho cha kisasa kikiwa hakijawahi kuonwa nchini, achilia mbali kuletwa  kwa umahiri wake uwanjani katika kulichezea gozi la ng’ombe.

Kwa waliomuona uwanjani na waliocheza na baba huyo wa Msemaji wa zamani wa Simba aliyepo Yanga kwa sasa, Haji Manara ni kwamba Sunday alikuwa na akili kama za Computer kiasi cha kushangaza na hata leo kuna watu wanakiri kwamba hakujawahi kutokea mchezaji aliyekuwa na kipaji cha kipekee yeye (Sunday).

John Makelele ‘Zigzag’ Mashabiki wa Simba na Yanga ni vigumu kulisahau jina hili, japo kila mmoja analikumbuka kwa aina tofuati na walichofanyiwa na straika huyu wa zamani wa Pamba-Mwanza.

John Makelele alibatizwa jina la Zig-Zag kwa aina ya uchezaji uliokuwa ukisumbua mno mabeki kwani hakuwa anatulia mstari mmoja. Makelele alikuwa akikimbia na kuwatambuka mabeki wa timu pinzani kwa mtindo wa zigzag kiasi ilikuwa ngumu kukabika huku akiwatungua makipa hodari kwa michomo ya aina yake.

SALUMU KABUNDA ‘Ninja’ Achana kabisa na beki huyo wa kati aliyewahi kutamba mabingwa wa zamani wa soka wa Tanzania, Tukuyu Stars, Yanga na Taifa Stars alikuwa Ninja kweli.

Aina yake ya kukaba washambuliaji kwa kutumia kila aina ya kiungo chake na kuruka miguu kama wapiganaji wa Kininja, ilimfanya Kabunda kupata jina kubwa ndani na nje ya nchi.

Ninja ilikuwa sio ajabu kwake kukugandishia mguu pajani, ilimradi tu usilete madhara langoni mwake na kuisaidia timu alizochezea kupata mafanikio makubwa. Baadaye alikuwa mstaarabu akaitwa Msudani.

OMAR CHOGO ‘Chemba’ Beki wa zamani wa Simba hakuwa mtu wa mchezo mchezo. Alibatizwa jina la Chogo Chemba kwa sababu ya aina yake ya uchezaji hasa kuruka na kubinuka kwa mtindo wa chemba, kwa wanaojua sarakasi hilo sio neno geni.

Katika pambano la kihistoria la Simba na Yanga mwaka 1974 lililopigwa Nyamagana Mwanza, Chemba alisimama kama beki wa kati sambamba na Athuman Juma. Kwa waliomuona uwanjani, wanakiri Omar Chogo alikuwa sio beki wa mchezo katika kuzuia washambuliaji, huku wengine wakimuita Mluya Jitu la Kenya kwa namna alivyokuwa amejaliwa mwili na weusi wa rangi.

Zamoyoni Mogella ‘Golden Boy’ Utasema nini kwa straika huyu wa zamani wa Simba, Yanga na Taifa Stars na kucheza soka la kulipwa nje ya nchi ikiwamo majirani zetu wa Kenya.

Mogella alibatizwa jina la Golden Boy, kwa umahiri wake wa kusaka soka na kipaji kikubwa cha kufumania nyavu. Kila ulipokuwa ukilisikia jina la Mogella ndani ya 18 basi wewe ulipaswa kuhesabu bao. Inaelezwa jina hilo la Golden Boy mwaka 1981 katika michuano yua Kombe la Chalenji ambapo alikuwa akiingizwa dakika chache kabla ya mechi kumalizika na kufunga mabao muhimu.

Mechi hasa iliyozaa jina hilo ilikuwa dhidi ya Malawi ambapo aliingizwa uwanjani na zikiwa zimesalia dakika mbili aliifungia Stars bao la kusawazisha na kufanya matokeo kuwa 2-2. Hadi sasa hakujawahi kupatikana Golden Boy mwingine mkali wa mabao kama gwiji huyo.

Sanifu Lazaro ‘Tingisha’ Tingisha aliwatingisha kweli kwenye soka la Tanzania enzi zake. Straika huyo wa zamani wa RTC Kagera, Yanga, Kajumulo World Soccer na Taifa Stars alitisha kwa umahiri wake uwanjani.

Winga  huyo aliwatingisha mabeki wa timu pinzani kiasi kwamba mwaka 1990 katika pambano la watani wa jadi, Simba na Yanga mashabiki waliamua kumbatiza jina hilo. Katika mechi hiyo Simba ililala mabao 3-1 na Tingisha akiwa amefunga moja ya mabao hayo, huku akiwaachia msala mabeki wa Simba kwa namna alivyokuwa akiwatambuka kwa chenga za maudhi na mbio na kupiga krosi zenye macho.

Makumbi Juma ‘Homa ya Jiji’ Wengine walikuwa wakimuita Bongabonga, mmoja wa washambuliaji hodari waliowahi kutokeas Tanzania. Makumbi aliyetokea Mkoa wa Kigoma na kutamba na timu za RTC Kigoma na baadaye Yanga na Taifa Stars alibatizwa jina la Homa ya Jiji kwa namna alivyokuwa akiwakosesha raha mashabiki wa Simba. Jamaa alikuwa anajua soka bwana na miguu yake ilikuwa na pua za kunusa nyavu ambapo ushirikiano wake na swahiba wake, Abeid Mziba ‘Tekero’ ulileta homa Msimbazi.

Wengine Orodha ya a.k.a za nyota wa zamani ni ndefu baadhi yao ni kama Mohammed Yahya’Tostao’, Kitwana Manara ‘Popat’, Abbas Dilunga ‘Sungura’, Abbas Said ‘Kuka’, Mohammed Kajole ‘Machela’, Athuman Juma Chama ‘Jogoo’, Rashid Idd ‘Chama’, Boi Idd ‘Wickens’, Edgar Mwafongo ‘Fongo’, Daud Salum ‘Bruce Lee’, Steven Mapunda ‘Garrincha’ , Jumanne Hassan ‘Masimenti’ na Said Sued ‘Scud’.

Pia, kulikuwa na Juma Pondamali ‘Mensah’, Maulid Dilunga ‘Mexico’ Mohammed ‘Bob’ Chopa, Godwin Aswile ‘Scania’, Malota Soma ‘Ball Juggler’, Frank Kassanga ‘Bwalya’, Juma Bakar ‘Kidishi’, Hassan Wazir ‘Wembe’, Said Mwamba ‘Kizota’, Said Mrisho ‘Zico wa Kilosa’ na Abubakar Salum ‘Sure Boy’.

Wapo kina Jimmy Mored ‘Moro’, Hamis Gaga ‘Gagarino’, Twaha Hamidu ‘Noriega’, Fred Felix ‘Minziro’, Ally Malilo ‘Loketo, Seif Khalfan ‘Bebeto’, Razak Yusuf ‘Careca’, Job Ayoub ‘Kwasakwasa’, Sunday Juma ‘Pikipiki’, Yasin Abuu ‘Napili’, Mohamed Rishard ‘Adolf’, Athuman Kilambo ‘Baba Watoto’, Omar Kapera ‘Mwamba’ na Mohammed Hashim ‘Mkweche’

Kulikuwa na kina Salum Mwinyimkuu ‘Carlos’, Elias Michael ‘Nyoka Mweusi’, George Kulagwa ‘Best’, Fumo Felician ‘Mwalimu’, Method Mogella ‘Fundi’, Itutu Kiggy ‘Road Master’, Omar Hussein ‘Keegan’, Isihaka Hassan ‘Chukwu’ na  Idd Seleman ‘Nyigu’ a.k.a Meya.

Pia, kulikuwa na kina Madaraka Seleman ‘Mzee wa Kiminyio’, Athuman Abdallah ‘China’ a.k.a Dynamo, Mao Mkami ‘Ball Dancer’, Joseph Kaniki ‘Golota’ a.k.a Kumbakumba, Mohammed Bakar ‘Tall’, Ezekiel Grayson ‘Jujuman’, Mohammed Hussein ‘Mmachinga’,  Razak Yusuf ‘Careca’, Abdallah Seifu ‘Kibadeni, King Mputa’  na wengineo kibao. NB: Mchezaji gani mwingine unayemkumbuka ambaye alikukosaha sana.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live