Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Boli la Kipre Jr lamkosha Dabo

Kipree  WA0003 Boli la Kipre Jr lamkosha Dabo

Sun, 26 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kocha Mkuu wa Azam FC, Youssouph Dabo amekiri kufurahishwa na kiwango kilichoonyeshwa na wachezaji wa kikosi hicho, huku akimmwagia sifa winga Kipre Junior aliyefunga hat-trick wakati wakiinyoa Mtibwa Sugar kwa mabao 5-0 kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara uliopigwa juzi usiku, jijini Dar es Salaam.

Katika mchezo huo, Azam ilipata mabao mengine kupitia kwa Lusajo Mwaikenda na Feisal Salum ‘Fei Toto’ ambaye pia aliasisti mara mbili na kumfanya afikishe asisti nne na kuhusika na mabao 10 ya Azam hadi sasa ikiwamo sita aliyofunga.

Akizungumza na Mwanaspoti, Dabo alisema ni jambo nzuri kuona wachezaji wote wakicheza vizuri na kufuata maelekezo yake huku akiweka wazi nyota wengi wa kikosi hicho kwa sasa wanaweza kuibeba timu migongoni mwao.

“Kipre anaendelea kuonyesha ubora wake ambao mashabiki wanataka kuuona kila siku, ni jambo nzuri kwa sababu inamuongezea hali ya kujiamini, niwapongeze wachezaji wote kwa kiwango bora walichokionyesha kwani ndivyo tunavyohitaji,” alisema Dabo.

Kipre aliyekuwa kwenye kiwango bora alipachika mabao hayo dakika ya 29, 43 na 63  na kumfanya sasa afikishe mabao manne kwenye orodha ya wafungaji. Hat trick hiyo ya juzi kwa Kipre inamfanya awe mchezaji wa nne msimu huu kufunga mabao matatu kwenye mechi moja akilingana na Fei Toto, Jean Baleke wa Simba na Stephane Aziz Ki wa Yanga.

Katika mchezo huo Mtibwa waliowahi kubeba ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara mbili mwaka 1999 na 2000 ilishindwa kabisa kuonyesha makali na kuzidi kujichimbia mkiani mwa msimamo ikizibeba timu 15 zilizopo juu yake, licha ya kushuka uwanjani mara 10 na kuvuna pointi tano hadi sasa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live