Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bodi yatamani VAR ije haraka Ligi Kuu Bara

VAR Yafungwa Mkapa Bodi yatamani VAR ije haraka Ligi Kuu Bara

Tue, 6 Feb 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Bodi ya Ligi (TPLB), imesema jambo linaloipasua kichwa kwa sasa ni kutegemea jicho la waamuzi kuchezesha mechi za Ligi Kuu Bara kwa asilimia 100.

Waamuzi wa ligi mbalimbali nchini wamekuwa wakinyooshewa vidole kwa kuboronga na kushindwa kutafsiri vyema sheria 17 za soka katika ligi zote zikiwemo za wilaya, mikoa, mabingwa wa mikoa (RCL), First league, Championship na Ligi Kuu Bara.

Mtendaji Mkuu wa Bodi hiyo, Almas Kasongo ameiambia Mwanaspoti kwamba eneo la waamuzi bado lina changamoto kubwa kwani soka limebaki na uamuzi wa kutegemea jicho lao kwa asilimia 100 na wanapokosea hakuna chombo kichonaweza kusahihisha kama wanaotumia VAR na vyombo vingine.

Alisema nchi zilizoendelea zimehamia kwenye uamuzi wa kisasa na waamuzi wanapata usaidizi wa video (VAR) pale wanapokosea au wanaposhindwa kuona tukio na vilevile usaidizi wa teknolojia ya goli (goal line technology).

“Eneo la uamuzi limebaki kuwa na changamoto siyo jana, leo hadi kesho hadi na sisi tutakapokuwa na vyombo vinavyosaidia waamuzi,” amesema Kasongo.

Ameweka wazi kuwa TPLB imekuwa ikitathmini kosa lolote la mwamuzi ili kutambua kama ni la makusudi, kupitiwa au la bahati mbaya, ili kuchukulia inapotokea makosa ambayo wengi huyaita kuwa ya kibinadamu.

“Hii ni changamoto kubwa kwetu kwa kuwa nchi zilizoendelea zina teknolojia kubwa ambayo inawasaidia kwenye uamuzi wao. Kuna VAR, lakini goal line technology ambazo zimekuwa zikitumiwa na wenzetu na tumeona zina mafanikio makubwa labda tutafika huko,” amesema.

Ametumia fursa hiyo kugusia mchezo wa Ligi ya Championship kati ya Mbuni FC dhidi ya TMA Stars ambao ulipigwa wikiendi iliyopita na kwamba watachukua video za mchezo huo na kuwapa wakufunzi wa waamuzi watakaozipitia na kuwashauri, na itakapobainika kulikuwa na makosa kamati itafanya uamuzi.

Mchezo huo uliopigwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha na kumalizika kwa sare ya 1-1 ulichezeshwa na mwamuzi wa kati Emmanuel Sonda kutoka Kigoma akisaidiwa na Ramadhani Kiloko na Mabrouk Abubakar wote kutoka Tanga.

Katika mchezo huo, Sonda aliwaonyesha kadi nyekundu mabeki wawili wa kati wa TMA Stars ambao ni Mhando Robert katika dakika ya 40 na Wilson Nangwa dakika ya 78 pamoja na kocha msaidizi wa Mbuni FC, Daniel Kirahi.

Sakata la waamuzi limekuwa la muda mrefu nchini na ni la kila upande wa Muungano, ambapo katika mashindano ya Kombe la Mapinduzi 2024 walisimamishwa kadhaa kutokana na makosa waliyoyafanya.

Hata hivyo, kwa upande wa Bara mashabiki na wapenzi wa soka wamekuwa wakilia na waamuzi kila mara na hasa katika michezo inayohusisha timu kubwa za Simba na Yanga, miongoni mwa madai yakiwa ni ya upendeleo dhidi ya vigogo hivyo.

Miaka miwili iliyopita mawaziri Dk Mwigulu Nchemba (Fedha) na Mohamed Mchengerwa aliyekuwa wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo waligusia mpango wa serikali kuleta teknolojia ya usaidizi wa uamuzi (VAR) ili kuwasaidia waamuzi kuamua mechi, lakini ahadi hiyo haikutekelezwa hadi Mchngerwa alipohamia Wizara ya Maliasili na Utalii kisha Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali (Tamisemi).

Chanzo: Mwanaspoti