Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bodi ya Ligi kukusanya maoni udhamini wa klabu

GSM X MO Bodi ya Ligi kukusanya maoni udhamini wa klabu

Fri, 23 Aug 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Bodi ya Ligi imesema kuwa inakaribisha maoni ya wadau wote ambao wanaona hakuna haja ya mtu, kampuni au taasisi kudhamini zaidi ya timu moja kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara ili iundwe kanuni rasmi.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa bodi hiyo, Almasi Kasongo, amesema jana kuwa, kwa siku za karibuni kumeibuka hoja na mjadala kwa wadau wa soka ambao wanadhani kuna haja ya kuzuia mdhamini mmoja kudhamini zaidi ya timu moja, na kwa kuwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi wanaendesha soka kwa uwazi na usikivu, hawajafunga milango badala yake wanakaribisha maoni.

Hata hivyo, Kasongo, amesema maoni hayo yatatolewa kwa ajili ya kanuni ya msimu ujao, kwani msimu huu tayari wameshafunga na hakukuwa na mdau yoyote aliyelalamikia suala hilo.

"Hizi siku mbili tatu umekuwa mjadala mkubwa, lakini kwa wakati huu tuliokuwa nao hakuna kanuni inayozuia mdhamini mmoja kudhamini zaidi ya timu moja.

Udhamini ni jambo la kikanuni, madhumuni ya kanuni kwa asilimia 90 yameelekezwa kwenye klabu husika, timu, wachezaji, waamuzi, viongozi, mbali na mijadala iliyoibuka, hakuna klabu yoyote au mdau kuelekea msimu huu aliyelalamikia suala hilo," alisema Ofisa Mtendaji huyo.

Hata hivyo, alisema kanuni siyo msahafu, hivyo kama wadau wataona kuna haja ya kuja na kanuni hizo, milango iko wazi.

"Lakini mimi siku zote nimekuwa nikiamini kuwa kanuni siyo msahafu, zinajadilika, zinabadilishika kwa hiyo pale ambapo wadau wataona kuna haja ya kufanya mabadiliko ya kanuni kama ambavyo siku zote tumekuwa tukifanya basi milango ipo wazi," alisema Kasongo.

Alisema wao kama viongozi wa soka, wataka kuongoza vile ambavyo wadau wa soka wataona inafaa na kuthamini michango yao.

Kwa siku za karibuni kumeibuka mijadala kwa wadau wa soka vikihusu uhalali wa mdhamini mmoja kudhamini zaidi ya klabu moja kwenye ligi moja.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: