Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bodi ya Ligi kufanyia maboresho kanuni

Almasi Kasongo Mtendaji Mkuu Bodi ya Ligi, Almasi Kasongo

Thu, 21 Jul 2022 Chanzo: www.mwananchi.co.tz

Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi (TPLB), Almas Kasongo amesema milango iko wazi kwa wadau wa soka kutoa maoni ya marekebisho ya kanuni ikiwamo michezo ya mchujo ambazo zilikuwa kilio msimu ulioisha.

Kauli ya Kasongo inakuja baada ya msimu uliomalizika wadau wengi kuonyeshwa kutoridhishwa ilivyotumika kupata timu zilizobaki Ligi Kuu Bara na zilizoshindwa kukata tiketi ya kupanda kutoka Championship.

Kanuni ya mchujo iliyotumika ni ile ya timu za Ligi Kuu Bara zilizomaliza nafasi ya 13 na 14 kucheza zenyewe na mshindi wa jumla kubaki kwa msimu ujao huku atayefungwa anacheza mchezo mmoja wa mwisho kuamua hatma yake na mshindi wa jumla wa Ligi ya Championship kati ya aliyemaliza nafasi ya tatu na ya nne kwenye msimamo.

Mtibwa Sugar (13) na Tanzania Prisons (14) ndizo timu za Ligi Kuu zilizocheza michezo ya mchujo na Mtibwa kushinda kwa jumla ya mabao 3-2. Kwa upande wa Championship zilikutana JKT Tanzania iliyomaliza ya nne na Kitayosce ya tatu kisha JKT kushinda kwa jumla ya 3-2.

Baada ya hapo ilizikutanisha Prisons ya Ligi Kuu Bara na JKT Tanzania kutoka Championship ili kutafuta timu itakayobaki na Prisons kusalia Ligi Kuu kufuatia ushindi wa jumla wa mabao 3-2 na JKT kuendelea kusalia Championship.

Akizungumzia hilo, kocha wa JKT Tanzania, Mohamed Abdallah ‘Bares’ alishauri timu tatu za Ligi Kuu zishuke moja kwa moja halafu mshindi wa jumla atakayemaliza nafasi ya tatu na nne kwenye Ligi ya Championship apande.

Alisema: “Tulicheza mechi mbili ‘play-off’ jambo lililotudhoofisha sana, hivyo ningeomba timu za Championship zikutane zenyewe kisha mshindi wa jumla akacheze Ligi Kuu. Hii itasaidia vijana wengi waliokuwa huku chini.”

Kocha wa Fountain Gate, Ahmed Soliman alisema mfumo wa sasa ni mzuri kwani unaleta ushindani mkubwa, ila angependekeza timu za Ligi Kuu na Championship zicheze zenyewe kwenye mchujo kupata mshindi wa jumla.

Chanzo: www.mwananchi.co.tz