Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bodi ya Ligi, kazi inaonekana

Almasi Kasongo India Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, Almas Kasongo

Sat, 8 Jul 2023 Chanzo: Mwanaspoti

HUU ni mwaka wa miaka10 tangu Bodi ya Ligi (TPLB) iliponzishwa ikichukua nafasi ya iliyokuwa Kamati ya Ligi katika Uendeshaji wa Ligi Kuu na Daraja la Kwanza (FDL) kwa Tanzania Bara.

Kuundwa kwa bodi hiyo kulikuwa ni matokeo ya harakati za uboreshaji katika uendeshaji wa soka nchini, lakini zaidi ya yote ni klabu za Ligi Kuu ziliweka presha kubwa kwa Shirikisho la Soka (TFF) kutaka uwepo wa chombo huru cha kuendesha ligi hiyo.

Juhudi kubwa za kuendesha soka kupitia chombo huru zilikuwa kwenye miaka ya 2010. Klabu za Ligi Kuu zilikuwa na malalamiko mengi kuhusu ligi ilivyokuwa ikiendeshwa na TFF, hasa katika masuala ya mapato na uamuzi.

Awali klabu zilianzisha Umoja wa Klabu za Ligi Kuu yaani miongoni mwa viongozi wake akiwa ni Mwenyekiti wa zamani wa Mtibwa Sugar ambaye pia aliwahi kuwa Makamu wa Rais wa TFF, Jamal Bayser. Nguvu ilikuja kuongezeka baada ya kuingia damu changa katika klabu z soka na ninaweza kusema vijana wale waliweka msukumo ambao TFF isingeweza kupindua mbele yao.

Katika umoja mpya wa klabu Mwenyekiti alikuwa ni Makamu wa Rais wa Simba, Geofrey Nyange 'Kaburu', huku makamu wake nikiwa mimi (Mwesigwa Selestine) wakati huo nikiwa Katibu Mkuu wa Yanga.

Tulikuwa nakundi la watu wengi wenye uwezo; nawakumbuka Patrick Kahemele, Said Tulliy, Idd Godigodi, Raheem Kagenzi 'Zamunda' na bila kumsahau marehemu Mzee Said Mohamed, aliyekuwa Mwenyekiti wa Azam FC.

Historia ni ndefu, lakini jambo linalofurahisha ni kuwepo kwa maendeleo chanya ya Bodi ya Ligi kuu kwani ligi imeendeshwa kwa amani kwa kiasi kikubwa kiasi kwamba matukio ya zamani kama ya timu kugomea mchezo kwa kupinga uamuzi yamepungua.

Sitaki kusema kuwa uamuzi umekuwa mzuri, hapana, ila kumekuwa na na ubora kulinganisha na hapo awali na pia taratibu za kupinga maamuzi zimekuwa na uwazi kwa kiasi fulani.

Wakati tunatafuta mfumo bora wa kuendesha ligi, kama klabu tulichangishana na kuleta wataalamu kutoka Marekani ambao walitusaidia mno katika hili.

Hivyo wakati TPLB inaundw tayari klabu zilijua zinataka nini na kwa kiasi kikubwa muundo wa uendeshaji umekidhi mahitaji ya wadau, japo haiwezi kuwa kwa asilimia 100. Hali ya utulivu na ushirikiano inaoupata bodi kutoka kwa wadau ni ushahidi tosha wa hilo.

Uwepo wa Televisheni ya michezo ya Azam umeiwezesha Bodi ya Ligi kujitangaza na kutangaza bidhaa yake kuu (Ligi) sokoni. Azam Pay TV ambao umri wake ni karibu sawa na umri wa bodi imekuwa mdhamini na pia promota mkubwa ligi.

Pamoja na Azam, wadhamini wengine kama Vodacom, KBC, NMB, DTB na NBC wamechangia katika kuwezesha Bodi ya Ligi kuwa imara, japo bado wadau wa soka wanaona bodi hiyo haina uhuru kama ilivyokuwa inapendekezwa wakati wa kuundwa kwao. Wengi wanaona kama inafanya mambo bila uhuru kwa kutegemea zaidi TFF na sio wao kama chombo huru kama bodi za nchi nyingine ikiwamo ile ya Kenya.

Ukimsifia mchimba msingi, msifie na mjenzi. Pamoja na juhudi kubwa za klabu na TFF kuanzisha Bodi ya Ligi, bodi hii kwa kiasi kikubwa imekuwa na bahati ya kuwa na uongozi imara tangu enzi za akina Wallace Karia, Said Mohamed na hadi sasa kwa Mwenyekiti Steven Mnguto na Mtendaji Mkuu, Almas Kasongo na uongozi bora unaonekana. Haishangazi kusikia kuwa Ligi Kuu Bara imezipiku ligi nyingi zilizokuwa mbele na sasa iko ndani ya nafasi 5 Bora Afrika.

Bado Bodi ya Ligi ina nafasi kubwa ya kufanya mengi kuendeleza mpira na kuongeza kipato. Ligi pia inaweza kushirikiana na kilabu na TFF kuendesha Ligi za Vijana kwa klabu na hata Ligi ya wachezaji wa akiba kama inavyofanywa kwa baadhi ya mataifa yaliyoendelea.

Pamoja na kwamba kanuni nyingi zakuendesha mpira zinatoka kwenye Kamati ya Utendaji ya TFF bado ligi ina nafasi ya kuwa chanzo cha utaratibu mzuri wa kutekeleza sera na kanuni za mashindano ya klabu.

Bodi ya Ligi ifanyie kazi tuhuma na malalamiko dhidi yao kama vile kucheleweshwa kwa posho za waamuzi na kuhakikisha kazi za waamuzi haziingiliwi na maslahi ya viongozi na hata klabu zinazoshiriki ligi.

Upangaji wa ratiba nao pia umelalamikiwa kuvipendelea baadhi ya klabu zenye nguvu ya fedha au nguvu ya ushawishi; hilo lisipofanyiwa kazi linaweza kuwaangusha.

Yote kwa yote, Bodi ya Ligi imefanikiwa kiasi cha TFF kujivunia kama moja ya mazao yake bora. Uendeshaji wa msimu wa Ligi wa 2022-2023 ni mfano wa mafanikio haya. Tunategeme mazuri kubebwa na mazuri zaidi kuingizwa katika msimu wa 2023-2024. Kila la kheri Bodi ya Ligi na hongereni TPLB.

Mwandishi wa makala hii ni Katibu Mkuu wa zamani wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF). Mtumie maoni yako kuhusu makala hii kwenye nambari yake ya simu hapo juu.

Chanzo: Mwanaspoti