Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bodi ya Ligi Kuu kuja na dawa wamiliki timu zaidi ya mbili

Almasi Kasongooo Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi hiyo, Almasi Kasongo.

Fri, 21 Jun 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Bodi ya Ligi Kuu imesema imeandaa mchakato wa kanuni kuzuia mtindo wa baadhi ya klabu kuhama mkoa mmoja kwenda mwingine katikati ya msimu pamoja na mtu au taasisi kumiliki timu zaidi ya moja kwenye Ligi Kuu.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi hiyo, Almasi Kasongo, amesema kazi hiyo inafanywa na Kamati ya Sheria ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), ambayo itatengeneza kanuni ya kuzuia tabia hiyo ya klabu kuondoka kwenye mkoa mmoja kwenda mwingine ndani ya msimu na kubadilishwa jina.

"Timu ilikuwa ya Mbeya, lakini ghafla imekuwa ya Shinyanga, mara inatoka Shinyanga inakwenda Tanga ndani ya msimu mmoja, hii si sawa, wenzetu wa Idara ya Sheria wanalifanyia kazi. Nafikiri sasa hivi tupo katika maboresho ya kanuni, watakuja na kitu ambacho kitamaliza kabisa au kupunguza mambo haya, " alisema Kasongo.

Msimu uliomalizika hivi karibuni klabu ya Singida Fountain Gate, ilihama kutoka Singida na kuhamia Mwanza, huku Ihefu ikihama kutoka Mbarali, Mbeya kwenda Singida.

Mbali na hilo, baadhi ya wachezaji wa Singida Fountain Gate nao walipelekwa kwenye klabu ya Ihefu ambayo kwa sasa imebadilishwa jina ikiitwa Singida Black Stars ambapo pia Ofisa Mtendaji huyo alisema kuwepo kwa kanuni itakayofanya kazi, ndiyo 'muarobaini' wa kuzuia mambo hayo.

Kuhusu mmiliki mmoja kuwa na timu mbili alisema lipo na limekuwa kilipigiwa kelele, lakini kwa bahati mbaya hawapati uthibitisho wowote wa kimaandishi kwenye hati ya umiliki.

"Hili la ndani ya ligi kuna mtu anamiliki zaidi ya klabu moja, tabu tunayoipata ukienda kwenye hati ya umiliki huioni, na huwezi kumpata na sisi tunafanya kazi kwa nyaraka siyo hisia, kisheria wanakushinda, lakini hili limezua mjadala mkubwa, sasa kuthibitisha ndiyo changamoto, lakini siyo kwamba wenzetu wa Idara ya Sheria wameliacha iendelee, hapana, bado wanatafuta namna ya kupambana nalo, ikiwemo kufuatiliwa mienendo yao ya kifedha ya klabu husika na wataalam wa kazi hizo, pamoja na chochote ambacho wataona kinaweza kuwawezesha kutambua mtu mmoja anajihusisha na klabu mbili kwenye ligi moja," alisema Kasongo.

Mbali na malalamiko hayo, pia kumeibuka maswali mengi juu ya udhamini wa klabu kwa kampuni au mtu mmoja kudhamini klabu zaidi ya moja ndani ya Ligi ambalo pia litafanyiwa kazi.

Kasongo, alisema wanaenda kufanyia kazi kila dosari walizoziona au au maeneo yanayopigiwa kelele na wadau ili kuwa na Ligi bora zaidi na imara.

Eneo lingine ambalo limekuwa likipigiwa kele na bodi hiyo ya Ligi imesema itaanza kutunga kanuni kudhibiti ni eneo la vitendo vya kishirikina na adhabu zake.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live