Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bocco misimu 16 ya kibabe, rekodi zampa heshima

Bpocco Misimu 16 John Bocco

Tue, 4 Jun 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Aliyekuwa mshambuliaji na nahodha wa Simba, John Raphael Bocco ‘Adebayor’, ametangaza rasmi kustaafu soka la ushindani baada ya kucheza kwa misimu 16 mfululizo huku akijitengenezea umaarufu mkubwa kuanzia ngazi ya klabu na timu ya Taifa.

Bocco amestaafu kucheza soka lakini wakati huo tayari ni kocha wa timu ya vijana ya Simba anayoendelea kuinoa na inaelezwa ataagwa rasmi na Wekundu wa Msimbazi hao kwenye tamasha la Simba Day lijalo.

Kutokana na kustaafu kwa Bocco aliyezichezea Azam, Simba na Taifa Stars kwa mafanikio, Mwanaspoti linakuletea rekodi za mshambuliaji huyo aliyeipandisha daraja Azam FC mwaka 2008.

MISIMU 16 YA KIBABE

Hadi nyota huyo anatangaza kustaafu kucheza soka, tayari ameitumikia Ligi Kuu Bara kwa misimu 16 mfululizo akianzia Azam FC kisha Simba.

Bocco ni miongoni mwa wachezaji watakaobaki katika historia ya Azam FC kwani aliyechangia timu hiyo kupanda rasmi Ligi Kuu Bara mwaka 2008 baada ya kuifunga Majimaji mabao 2-0 kwenye Ligi ya Taifa 2007, Uwanja wa Jamhuri Dodoma.

Timu hiyo ilianza kwa kutoka suluhu na Mbagala Market, ikaifumua Kijiweni mabao 3-0, kisha ikakutana na Majimaji katika mechi iliyopigwa Julai 27, 2007 huku mabao yote mawili yakiwekwa kimiani na mshambuliaji huyo tishio kikosini humo msimu huo.

Bocco kabla ya kujiunga na Azam, alikuwa akiichezea Cosmopolitan katika Ligi ya Mkoa wa Dar es Salaam na kiwango bora alichokuwa nacho msimu huo kiliwavutia mabosi wa kikosi hicho kumsajili ili kuongeza nguvu kwenye mechi za Ligi ya Taifa.

Katika misimu tisa ya nyota huyo, moja kati ya jambo ambalo ni la kukumbukwa ndani ya kikosi cha Azam ni kuipa ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa mara ya kwanza msimu wa 2013-2014 ikiwa ndio mara ya kwanza kwao na hadi leo wamekuwa wakiuota tu.

Mbali na ubingwa huo na mingineyo ambayo amechukua, ila amewahi pia kuibuka mfungaji bora akiwa na timu hiyo wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2011-2012 alipofunga jumla ya mabao 19, ikiwa ni rekodi iliyodumu kwa misimu 12 hadi kufikiwa msimu huu.

Mabao 19 ya nyota huyo yamedumu kwa muda mrefu bila kufikiwa au kuvunjwa na mchezaji yoyote ndani ya kikosi hicho hadi ilipotokea msimu uliopita baada ya kufikiwa na kiungo mshambuliaji, Feisal Salum ‘Fei Toto’ aliyefunga idadi kama hiyo.

Kiwango bora alichokionyesha ndicho kilichowavutia mabosi wa Simba kumsajili msimu wa 2017-2018 akiwa sambamba na nyota wengine wakiwemo kipa, Aishi Manula na beki wa kulia, Shomari Kapombe na kiungo kiraka, Erasto Nyoni aliyepo Namungo kwa sasa.

Katika misimu saba Bocco akiwa na kikosi cha Msimbazi, amenyakua mataji manne ya Ligi Kuu Bara mfululizo baada ya timu hiyo kusota miaka mitano, Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) mara mbili, Ngao ya Jamii mara nne na Kombe la Mapinduzi mara moja.

Mbali na hilo, ila ameibuka pia mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2020-2021 akiwa na kikosi hicho akifunga jumla ya mabao 16 akimpiku dakika za mwishoni aliyekuwa mshambuliaji mwenzake wa timu hiyo, Chris Mugalu aliyemaliza na 15.

MFUNGAJI BORA MUDA WOTE

Kama hujui ni kwamba Bocco ndiye mfungaji bora wa muda wote wa Ligi Kuu Bara baada ya kuipiku rekodi ya Mohammed Hussein ‘Mmachinga’.

Bocco kwa sasa amefikisha jumla ya mabao 154 katika Ligi Kuu Bara na 84 aliyafunga akiwa na Azam FC na mengine 70 akifunga na Simba huku Mmachinga aliyechezea timu za Bandari Mtwara, Yanga, Simba, Mmbanga na Twiga Sports akifunga 153.

Mmachinga aliyecheza Ligi Kuu Bara kwa misimu 13, ndiye aliyekuwa anashikilia rekodi ya mfungaji bora wa muda wote kabla ya Bocco kuivunja japo inayoendelea kuwatesa nyota wengi ni ile ya mwaka 1998 alipotupia mabao 26, inayoendelea kuishi.

Akimzungumzia Bocco, aliyekuwa kocha mkuu wa timu hiyo Mbrazili, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ alisema, moja ya jambo kubwa alilokuwa akifurahia kufanya kazi na mshambuliaji huyo ni kutokana na nidhamu nzuri aliyokuwa nayo kikosini.

“Kila kocha hupenda kufanya kazi na mchezaji anayezingatia na kufuata maelekezo anayotoa kwa ufasaha, Bocco ni zaidi ya kiongozi uwanjani, ndiyo maana kuna muda mashabiki walikuwa wanapiga kelele sana asicheze ila sikuzingatia matakwa yao.”

Aliyekuwa kocha wa Simba, Patrick Aussems ‘Uchebe’ alisema Bocco alikuwa mchezaji kiongozi na mshambuliaji bora aliyekuwa na mapenzi na timu.

“Bocco ni moja ya manahodha wazuri niliofanya nao kazi, ni mtu imara katika maamuzi pia kufikisha ujumbe kwa wenzake na kusimamia kuhakikisha malengo yanatimia,” alisema Aussems.

Beki wa Singida Fauntain Gate, Abdul Majid Mangalo alimzungumzia Bocco kama mchezaji kiongozi huku akisimulia moja ya jambo alilowahi kumkanya Septemba 20 kwenye mechi wakati akiwa nahodha wa Biashara United baada ya kuchezewa rafu na Meddie Kagere na kuwa na jazba kali iliyotulizwa na Bocco.

“Ilikuwa hivi, nilishika mpira wakati wachezaji wengine wanabishana, kumbe Kagere alikuwa nyuma yangu akaupiga bahati mbaya ukanigonga usoni hadi nikaanguka, nikadhani kanipiga ngumi, nilipoinuka kwa jazba Bocco aliona akanifuata kwa uharaka na kunivutia pembeni;

“Akaniuliza dogo una shida gani inayokufanya utake kuharibu tabia yako! Nikamwelezea kilichotokea, akanishika mkono hadi kwa Kagere ambaye hata hivyo, alijishusha na kuniambia lengo lake lilikuwa kuupiga mpira uendelee na sio kuniumiza, kisha Bocco akaniambia mdogo wangu usitatue matatizo kwa jazba badala yake uwe muumini wa kazi nzuri na nidhamu uwanjani,” alisema na kuongeza:

“Ni mara kadhaa Bocco nikikutana naye uwanjani ananiambia nina kipaji nikitunze kwa nidhamu, kiukweli ni mchezaji anayependa wengine wafanikiwe na ndivyo nahodha anatakiwa awe kiongozi wa mfano.”

Kwa upande wa beki wa Namungo, Frank Magingi alisema Bocco ana nidhamu hadi kwa timu pinzani kuhakikisha soka linachezwa bila vurugu na hata akikosewa ni mwepesi wa kusamehe.

“Bocco ndani yake ana hekima kubwa, ukimkosea hawezi kukufuata kwa hasira anakuelekeza soka ni amani, pia akiona una kitu anakushauri namna ya kuhakikisha unakuwa bora, kiukweli anastahili kuwa kiongozi wa wengine,” anasema Magingi.

MABAO YAKE LIGI KUU AZAM FC

2008/2009=1

2009/2010=14

2010/2011=12

2011/2012=19

2012/2013=7

2013/2014=7

2014/2015=2

2015/2016=12

2016/2017=10

JUMLA=84

SIMBA

2017/2018=14

2018/2019=16

2019/2020=9

2020/2021=16

2021/2022=3

2022/2023=10

2023/2024=2

JUMLA=70

AZAM FC + SIMBA SC=154

MATAJI YAKE LIGI KUU BARA (5)

-2013-2014 (Azam FC)

-2017-2018 (Simba)

-2018-2019 (Simba)

-2019-2020 (Simba)

-2020-2021 (Simba)

KOMBE LA FA (2)

-2019-2020 (Simba)

-2020-2021 (Simba)

NGAO YA JAMII (4)

-2018 (Simba)

-2019 (Simba)

-2020 (Simba)

-2023 (Simba)

KOMBE LA MUUNGANO (1)

-2024 (Simba)

KOMBE LA MAPINDUZI (1)

-2022 (Simba)

MFUNGAJI BORA (2)

-2011-2012 (Azam FC)-Mabao 19

-2020-2021 (Simba)-Mabao 16

Chanzo: Mwanaspoti