Kipa Beno Kakolanya ameishika pabaya Simba wakati mkataba wake ukiwa ukingoni na tayari kukiwa na taarifa ameshamalizana na mabosi wa Singida Big Stars ili kujiunga nao kwa msimu ujao, lakini vigogo wa Msimbazi hawajakubali kirahisi kwa kuamua kumtumia John Bocco kuingilia kati.
Kakolanya aliyeanza mazungumzo ya awali na Simba kabla ya kukwama kutokana na dau alilowekewa mezani ili kusaini mkataba mpya, huku ikidaiwa ameshapata dili jipya la Singida akiwekewa zaidi ya Sh 100 Milioni kiasi cha kuwachanganya mabosi wa Msimbazi na kuamua kumrudia upya wajadiliane.
Katika kuhakikisha wanamlainisha kipa huyo wa zamani wa Tanzania Prisons na Yanga mabosi wa Simba wameamua kumtumia nahodha wa timu hiyo, John Bocco kuzungumza naye na inaelezwa jamaa amelainika, lakini iwapo kama atapewa Sh 170 milioni
Awali inaelezwa Kakolanya alikuwa kwenye mazungumzo mazito na Mtendaji Mkuu wa Simba, Imani Kajula lakini hata hivyo, hawakufikia muafaka na kutokana na ugumu wa ratiba ya Simba kwa wiki za hivi karibuni.
Chanzo cha kuaminika ndani ya Simba, kimeeleza sakata la mchezaji huyo kwa sasa limeingiliwa na Bocco pamoja na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa klabu hiyo, Salum Abdallah 'Try Again' kila mmoja kwa wakati wake waliongea na kipa huyo ili kuona kama kuna uwezekano wa kumbakisha kikosini kwa kumtimizia mahitaji yake.
"Hakuna ambaye anatamani kuona Beno (Kakolanya) anaondoka Simba kwani ni kipa mzoefu na mwenye uwezo mkubwa licha ya kwamba sio chaguo la kwanza, lakini naona suala lake ni gumu kwa sababu kiasi ambacho anahitaji ni tofauti na kile ambacho wamepanga kumpa," kilisema chanzo makini kutoka ndani ya Simba na kuongeza;
"Naona kama suala lake limekuwa gumu, lilianzia kwa Mtendaji Mkuu na sasa limefika kwa Try Again na Bocco alijaribu kuongea naye, lakini amesimamia msimamo wake akitaka kutekelezewa dau alilolitaka ambalo ni zaidi ya Sh 100 Milioni."
Tayari Beno amewaeleza mahitaji yake hivyo kilichobaki ni viongozi kutafakari juu ya suala hilo na kufanya maamuzi kabla ya mkataba wake haujafikia ukomo, huku klabu ya Singida ikitajwa kumnyemelea.
Akizungumzia juu ya dili hilo la Kakolanya kutaka kutua Singida, kocha wa timu hiyo, Hans van der Pluijm alisema; "Malengo ni kucheza msimu ujao michuano ya kimataifa, ikiwa tutafanikisha hilo ndio tunaweza kuongea vizuri juu ya usajili."
"Nisikudanganye kwa sasa tupo bize juu ya namna ya kumaliza vizuri msimu, wachezaji ni mengi ambao wanatamani kucheza Singida lakini hiki sio kipindi cha kuongelea hilo," alisema Mholanzi huyo kwa msisitizo.
Mbali na kutumika kama mbadala wa Aishi Manula kwenye michezo mingi ya Ligi Kuu Bara na Ligi ya Mabingwa Afrika, Beno amepata nafasi msimu huu kucheza michezo yote ya Simba upande wa Kombe la Azam Sports Federation Cup (ASFC) na hajaruhusu bao.