Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bingwa Ligi Kuu Zanzibar sasa kujulikana Ijumaa

KVZ Zanzibar Bingwa Ligi Kuu Zanzibar sasa kujulikana Ijumaa

Wed, 19 Jun 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Ligi Kuu ya Zanzibar msimu wa 2023/24 inatarajia kufika tamati Ijumaa wiki hii na kumpata bingwa atakayeiwakilisha Zanzibar katika michuano ya Ligi ya Mabigwa Afrika.

Ligi hiyo ambayo kwa sasa ipo katika mzunguko wa 29 imebakiza mzunguko mmoja ili kukamilika kwa msimu.

Hata hivyo, bado ni vigumu kutabiri timu itakayoweza kutwaa ubingwa huo kutokana na timu mbili za juu katika msimamo, JKU na Maafande wa Zimamoto, kila moja kuwa katika nafasi nzuri ya kulibeba taji hilo.

JKU ipo kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 62 ikifuatiwa na Maafande wa Zimamoto wenye alama 61, hivyo mechi za mwisho ndizo zitakazoamua timu itakayotwaa ubingwa msimu huu.

Mabingwa watetezi wa ligi hiyo, KMKM SC, tayari wameshapoteza nafasi ya kutetea taji hilo kutokana na kushika nafasi ya tatu kwenye msimamo kwa kujikusanyia pointi 54 hadi sasa.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Bodi ya Ligi ya Shirikisho la Soka la Zanzibar (ZFF), mzunguko wa 29 wa ligi hiyo utaendelea leo kwa kupigwa michezo ambayo huenda ikaamua Bingwa wa Ligi Kuu ya Zanzibar.

Vinara JKU watashuka uwanjani kuvaana na KMKM katika Uwanja wa Amaan B wakati Zimamoto wenyewe watavaana na wakongwe Mlandege FC katika dimba la Mau A.

Kwa upande wa timu ambazo zinapambana kubaki Ligi Kuu, utapigwa mchezo mmoja ambapo Malindi SC watavaana na New City FC katika Uwanja wa Mau B.

Katika mechi za mzunguko wa 29 zilizopigwa juzi timu ya Mafunzo ilitoshana nguvu na Kipanga FC kwa kufungana mabao 3-3 mchezo uliopigwa Uwanja wa Mau A, wakati Kisiwani Pemba katika Uwanja wa FInya, Jamhuri SC na Chipukizi FC nazo zilitoka sare ya bao 1-1.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live